Na John Walter -Babati
Imeelezwa kuwa maziwa ya mama ni chakula cha kwanza, salama na chenye virutubisho vyote muhimu anavyohitaji mtoto katika miezi sita ya mwanzo ya maisha yake.
Hayo yameelezwa wakati wa kilele cha Wiki ya Unyonyeshaji Duniani katika Halmashauri ya Wilaya ya Babati, kilichofanyika katika Kijiji cha Magugu, ambapo jamii imepewa elimu kuhusu umuhimu wa unyonyeshaji wa maziwa ya mama kwa afya na ukuaji wa mtoto.
Kwa mujibu wa wataalamu wa afya na lishe, mama anatakiwa kumnyonyesha mtoto maziwa ya mama pekee kwa kipindi cha miezi sita ya mwanzo ya maisha yake, bila kumpa maji, chakula au kinywaji kingine, isipokuwa pale ambapo kuna maelekezo maalum ya kitabibu.
Kaulimbiu ya Wiki ya Unyonyeshaji Duniani mwaka 2026 ni: “Mwanzo Imara wa Maisha ya Mtoto, Huanza na Maziwa ya Mama,” ikisisitiza umuhimu wa kuhakikisha kila mtoto anaanza maisha akiwa na msingi bora wa afya kupitia unyonyeshaji sahihi.
Halmashauri ya Wilaya ya Babati imeendelea kutoa elimu ya unyonyeshaji kwa akina mama kuanzia wanapohudhuria kliniki wakati wa ujauzito hadi baada ya kujifungua, ikiwa ni sehemu ya juhudi za kuimarisha afya ya mama na mtoto pamoja na kuzuia changamoto za utapiamlo na udumavu.
Akizungumza katika kilele hicho, Aliche Mwalo, Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Babati ambaye pia ni Afisa Elimu Sekondari, akiwa Mgeni Rasmi, amesisitiza umuhimu wa jamii kuendelea kupata elimu kuhusu lishe na malezi bora ya watoto.
Kwa upande wake, Mganga Mkuu wa Halmashauri ya Wilaya ya Babati ameitaka jamii kujifunza zaidi kuhusu masuala ya lishe ili kuepuka changamoto za utapiamlo na udumavu kwa watoto.
Aidha, akina baba wametakiwa kuwa mstari wa mbele kumsaidia mama anayenyonyesha, kwa kuhakikisha anapata chakula bora na chenye virutubisho, mazingira ya utulivu pamoja na kumpunguzia majukumu mazito ya kazi za nyumbani ili aweze kupata muda wa kutosha wa kunyonyesha mtoto.
Afisa Lishe wa Halmashauri ya Wilaya ya Babati, Erick Bunziya Peter, amewataka akina mama kuzingatia unyonyeshaji wa maziwa ya mama pekee kwa miezi sita ya mwanzo ya maisha ya mtoto, akisisitiza kuwa hatua hiyo ni muhimu katika kumjengea mtoto msingi bora wa afya na ukuaji.
Amesema jamii inapaswa kuendelea kushirikiana katika kuhakikisha mama anayenyonyesha anapata msaada unaohitajika, kwani malezi na lishe bora ya mtoto ni jukumu linalohitaji ushiriki wa familia na jamii kwa ujumla.
Wiki ya Unyonyeshaji Duniani inaendelea kuwa fursa muhimu ya kuelimisha jamii kuhusu umuhimu wa maziwa ya mama na kuhamasisha familia, hususan akina baba, kushiriki kikamilifu katika kuhakikisha mama anayenyonyesha anapata mazingira bora ya kumhudumia mtoto.
