Mbunge wa jimbo la Arumeru Magharibi Dkt.Johannes Lukumay akizungumza na waandishi wa habari mara baada ya kutembelea mabanda mbalimbali katika maonesho ya nanenane Njiro.

Mkurugenzi wa halmashauri ya wilaya ya Arusha ,Suleiman Msumi akizungumza katika banda hilo nanenane Njiro

………..
Na Happy Lazaro, Arusha
Mbunge wa Jimbo la Arumeru Magharibi ,Dkt.Johannes Lukumay amesema Serikali inayoongozwa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan imeendelea kuweka nguvu kubwa katika sekta ya kilimo kwa kutoa ruzuku ya mbegu na mbolea kwa wakulima, hatua ambayo imeelezwa kuwa na mchango mkubwa katika kuongeza uzalishaji na kipato cha wananchi.
Akizungumza katika Maonyesho ya Nanenane baada ya kutembelea mabanda mbalimbali likiwemo la halmashauri ya Arusha,Dkt .Lukumay amemshukuru Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kuwekeza katika kilimo na kuboresha maisha ya wananchi, ambapo jimbo la Arumeru Magharibi limepokea uwekezaji mkubwa kupitia programu za ruzuku.
Amesema katika kipindi cha mwaka uliopita, zaidi ya Shilingi bilioni 17 zilitengwa kwa ajili ya ruzuku ya mbegu, huku kiasi cha Shilingi bilioni 3 kikielekezwa kwenye ruzuku ya mbolea, hivyo kufanya jumla ya uwekezaji huo kufikia zaidi ya Shilingi bilioni 20.
Dkt .Lukumay amepongeza jitihada zinazofanywa na Halmashauri hiyo katika kuwawezesha wananchi kiuchumi, hususani wanawake, kupitia mikopo yenye masharti nafuu.
Amesema baadhi ya vikundi vya wanawake vimepata mikopo yenye riba ya asilimia nne na kuanzisha miradi mbalimbali ikiwemo uzalishaji wa mazao ya kilimo na ufugaji wa nyuki.
“Nampongeza Mkurugenzi wa Halmashauri hii kwa kuhamasisha wananchi kutumia fursa za mikopo hiyo na napenda kutumia fursa hii kuwataka wataalamu wa kilimo kuendelea kutoa elimu kwa wakulima ili waweze kunufaika kikamilifu na programu za Serikali.”amesema Dkt.Lukumay.
Aidha amesisitiza umuhimu wa wakulima kusajiliwa katika mifumo rasmi ya Serikali huku akisema hatua hiyo itawarahisishia kupata ruzuku ya mbegu na mbolea pamoja na huduma nyingine za kilimo.
Dkt.Lukumay amefafanua kuwa,usajili utawawezesha wakulima kupata taarifa na elimu kuhusu mbinu bora za uzalishaji ili kuongeza tija na ubora wa mazao.
Aidha Dkt Lukumay amewapongeza wataalamu wa kilimo waliopo katika jimbo hilo kwa kuendelea kuwafikia wakulima katika maeneo yao na kutoa elimu inayolenga kuboresha uzalishaji.
Amesema Maonyesho ya Nanenane ni fursa muhimu kwa wakulima kupata elimu, kujifunza teknolojia mpya na kufahamu fursa mbalimbali zinazopatikana katika sekta ya kilimo, huku akiwataka wananchi kutumia fursa hizo kwa ajili ya kuongeza uzalishaji na kuboresha maisha yao.
Naye Mkurugenzi wa halmashauri ya Arusha ,Msumi amewataka wakulima na wafugaji kuchangamkia fursa za kilimo na mikopo kwa ajili ya kujikwamua kiuchumi.
Msumi amesema kuwa, serikali inaendelea kuweka mkazo katika kuboresha shughuli za kilimo na ufugaji kwa lengo la kuongeza uzalishaji, kipato na kujitegemea kwa wananchi, hususani wakulima na wafugaji.
Msumi amesema kuwa, Halmashauri hiyo imeshiriki katika maonyesho hayo kupitia sekta za kilimo na mifugo, ikiwa na mabanda mawili kwa ajili ya kutoa elimu na kuonesha shughuli mbalimbali zinazofanywa na wananchi.
Amesema kupitia ushauri wa kitaalamu unaotolewa na maafisa ugani na maafisa mifugo, baadhi ya wafugaji wameanza kutumia mbinu za kisasa za ufugaji, jambo ambalo limeongeza tija na kuboresha uzalishaji wa mifugo.
Aidha, amesema kumekuwa na mabadiliko makubwa katika kilimo cha mbogamboga, ambapo wakulima wameweza kuongeza uzalishaji na kipato, na hivyo kupunguza utegemezi wa kipato cha kawaida.
“Baadhi ya wakulima pia wamefanikiwa kutambuliwa na kupewa zawadi kutokana na ubunifu na mafanikio yao katika shughuli za kilimo.”amesema Msumi.
Aidha amewataka wakulima na wafugaji kutumia kikamilifu fursa zinazotolewa na maafisa ugani na maafisa mifugo katika kata zao, kwa kuhudhuria mafunzo na kupata elimu ya kitaalamu itakayowawezesha kuongeza uzalishaji na kipato.
