Mkurugenzi wa Idara ya Usimamizi wa Mali za Serikali, Wizara ya Fedha, Bw. Chotto Sendo, akizungumza na Baadhi ya Watumishi wa Wizara ya Fedha, alipowatembelea katika Banda la Wizara ya Fedha, wakati wa Maonesho ya Kimataifa ya Kilimo (Nanenane), yaliyofanyika katika Uwanja wa Dkt. John Samwel Malecela, Nzuguni jijini Dodoma.

Mkurugenzi wa Idara ya Usimamizi wa Mali za Serikali, Wizara ya Fedha, Bw. Chotto Sendo, akiagana na Afisa Habari Mwandamizi, Wizara ya Fedha, Bw. Ramadhani Kissimba, mara baada ya kutembelea Banda la Wizara ya Fedha, wakati wa Maonesho ya Kimataifa ya Kilimo (Nanenane), yaliyofanyika katika Uwanja wa Dkt. John Samwel Malecela, Nzuguni jijini Dodoma. (Picha na Kitengo Cha Mawasiliano Serikalini, WF- Dodoma)
…………….
Na. Asia Singano na Josephine Majura, WF – Dodoma
Serikali imezitaka taasisi zote za umma nchini kuimarisha usimamizi wa mali za Serikali kwa kuhakikisha taarifa zote za mali zinaingizwa na kutunzwa katika Mfumo wa Serikali wa Usimamizi wa Mali (GAMIS), ili kuongeza uwajibikaji, kuimarisha matumizi ya rasilimali za umma na kupunguza hoja za ukaguzi.
Maagizo hayo yalitolewa na Mkurugenzi wa Idara ya Usimamizi wa Mali za Serikali, Wizara ya Fedha, Bw. Chotto Sendo, alipotembelea Banda la Wizara ya Fedha, wakati wa Maonesho ya Kimataifa ya Kilimo (Nanenane), yaliyofanyika katika Uwanja wa Dkt. John Samwel Malecela, Nzuguni jijini Dodoma.
Alisema Serikali imetumia fedha nyingi kuwekeza katika miradi ikiwemo ujenzi wa mradi wa kufua umeme wa Bwawa la Mwalimu Nyerere -JNHPP (takribani sh. trilioni 6), ujenzi wa Reli ya kisasa-SGR (takribani sh. trilioni 10.6), ununuzi wa ndege, ujenzi wa Daraja la Kigongo-Busisi (takribani sh. bilioni 716.3) pamoja na utekelezaji wa miradi ya maji mijini na vijijini (takribani sh. bilioni 457.4), huku akisisitiza umuhimu wa miradi hiyo.
“Mali za umma ni rasilimali muhimu zinazowezesha Serikali kutoa huduma kwa wananchi na kutekeleza miradi ya maendeleo, huku wastani wa asilimia 70 ya bajeti za taasisi za umma ukitumika katika ununuzi unaozalisha mali hizo, usimamizi wake unapaswa kuzingatia uwajibikaji, ufanisi na utii wa sheria, kanuni na taratibu zilizowekwa’’ alisema Bw. Sendo.
Alisisitiza kuwa kutokana na uwekezaji mkubwa na wingi wa rasilimali nchini ni muhimu kuwa na mikakati madhubuti ya kuzisimamia mali hizo ili ziweze kutumika kwa matumizi yaliyokusudiwa na kuiwezesha Serikali kupata manufaa ya uwekezaji uliokusudiwa kwa kipindi kirefu.
‘’Kwa upande wa Wizara ya Fedha ikiwa na dhamana ya Usimamizi wa Mali za umma nchini imefanya jitihada mbalimbali katika kuongeza ufanisi wa Usimamizi wa Mali za umma nchini kwa Kusimika na kuwezesha matumizi ya mfumo wa Kielektroniki wa Usimamizi wa Mali za Serikali
“Government Assets Management Information Systems – (GAMIS) ambao unatumika kutunza na kuchakata taarifa za mali za Taasisi zote za Umma hapa nchini’’, alisema Bw. Sendo.
Aliongeza kuwa, Wizara ya Fedha imefanya maboresho katika Sheria ya Fedha za Umma sura 348 pamoja na kuandaa Kanuni mahususi za Usimamizi wa Mali za Umma za mwaka 2024 ikiwa ni utekelezaji wa azma ya kuimarisha Mifumo ya Usimamizi wa Mali za Umma nchini.
Alisisitiza Maafisa Masuuli kuwa na mifumo thabiti ya uwajibikaji na kuwa mfano bora kwa wengine kwa kuzingatia misingi ya uadilifu, uwajibikaji, uwazi, na ufanisi katika kuonyesha kwamba mali za umma ni amana ambayo wamekabidhiwa kwa niaba ya Watanzania wote.
Aidha, taasisi hizo zimetakiwa kuhakikisha mali chakavu, sinzia, ziada na zilizokwisha muda wa matumizi zinaondoshwa kwa kuzingatia sheria, kanuni na miongozo iliyopo ili kuimarisha ufanisi wa matumizi ya mali za umma.
Katika hatua nyingine Bw. Sendo amezitaka taasisi za umma kuwasilisha taarifa za ajali, hasara na upotevu wa mali kwa Mlipaji Mkuu wa Serikali ndani ya siku 30 tangu tukio litokee na mali zilizopata ajali au uharibifu zifanyiwe matengenezo mara baada ya kupata kibali husika.
