Happy Lazaro,Arusha .

Arusha: Wananchi wa Arusha wameaswa kuhakikisha mazao, mifugo, mali na biashara zao zinalindwa kwa bima, ili kupunguza athari za majanga na hasara zinazoweza kujitokeza.

Akizungumza katika Maonesho ya Nanenane Arusha, Meneja wa TIRA Kanda ya Kaskazini, Dkt. Emmanuel Lupilya, amesema wananchi wanapaswa kuichukulia bima kama sehemu muhimu ya kulinda jasho na uwekezaji wao.

Dkt. Lupilya amesema TIRA pamoja na registrants wake wapo Nanenane kutoa elimu na kuwawezesha wananchi kuelewa bidhaa mbalimbali za bima zinazoweza kuwalinda dhidi ya hatari katika kilimo, mifugo, biashara na mali.

“Bima si kusubiri tatizo litokee; ni maandalizi kabla tatizo halijatokea. Kila mbegu ikipandwa ilindwe, kila jasho lilindwe, na kila mali iwe na kinga ya bima,” amesema Dkt. Lupilya.”

Amewataka wananchi kutumia fursa ya Nanenane kuuliza, kujifunza na kupata huduma sahihi za bima kutoka kwa registrants waliopo katika maonesho hayo.

“Tupo hapa kuhakikisha wananchi hawapotezi jasho lao bure. Kilimo kikikua, biashara zikikua na mali zikiongezeka, ulinzi wa bima nao lazima ukue,” ameongeza.