Tanzania, wadau waimarisha ushirikiano utekelezaji wa malengo ya hifadhi ya bioanuwai

Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania itanufaika na Ushirika wa Wadau wa Hifadhi ya Bioanuwai kwa kupata fedha, teknolojia na kujengewa uwezo wa kitaalam. 

Hayo yamebainishwa kupitia mazungumzo kati ya Katibu Mkuu, Ofisi ya Makamu wa Rais na wawakilishi wa NBSAP Implementation Partners, wakiwemo wawakilishi kutoka Shirika la Umoja wa Mataifa la Mazingira (UNEP), NBSAP Accelerator Partnership, NBSAP Mainstreaming Initiative na Sekretarieti ya Mkataba wa Umoja wa Mataifa wa Hifadhi ya Bioanuwai (CBD Secretariat).

Mkutano huo umefanyika pembezoni mwa mikutano ya SBSTA 28 na SBI 7 jijini Nairobi, Kenya ambapo upande wa Wadau uliwakilishwa na Bi. Catherine Madden, Bi. Linda Kruger, Bi. Adri Rivera na Bw. Antony Kamau.

Mazungumzo hayo yamelenga kuimarisha ushirikiano wa Tanzania na washirika hao katika kuharakisha utekelezaji wa Mkakati na Mpango Kazi wa Taifa wa Hifadhi ya Bioanuwai (NBSAP) 2025–2030, ambao umehuishwa na kuoanisha malengo ya Taifa na Malengo ya Kunming–Montreal ya Kuhifadhi Bioanuwai Duniani (KM-GBF). 

Aidha, Katibu Mkuu amesisitiza kuwa baada ya Tanzania kukamilisha NBSAP, kipaumbele sasa ni kuhakikisha malengo yaliyowekwa yanatafsiriwa na kuwa matokeo yanayoonekana.

Katika mazungumzo hayo, Dkt. Muyungi ameeleza kuwa NBSAP 2025–2030 imeweka malengo mbalimbali, yakiwemo kupunguza upotevu wa bioanuwai kwa angalau asilimia 30 katika maeneo ya nchi kavu ifikapo mwaka 2030; kuchangia kufikia lengo la “30×30” la kuhifadhi asilimia 30 ya maeneo ya nchi kavu na bahari; pamoja na kuhamasisha angalau Dola za Marekani milioni 300 kwa mwaka kutoka vyanzo vya umma na sekta binafsi kwa ajili ya utekelezaji wa NBSAP.

Katibu Mkuu amebainisha kuwa Tanzania inahitaji kuimarisha zaidi ushirikiano na washirika katika uhamasishaji wa rasilimali fedha, kujenga uwezo wa kitaalam, kuimarisha mifumo ya ukusanyaji na matumizi ya takwimu za bioanuwai, pamoja na kuingiza masuala ya bioanuwai katika sekta muhimu za uchumi, hususan kilimo, uvuvi, utalii na nishati.

Kwa upande wa UNEP, Tanzania imeshukuru msaada wa kitaalam uliotolewa wakati wa kuhuisha NBSAP kupitia mradi wa Early Action Support na kuomba ushirikiano zaidi katika kuandaa viashiria mahsusi vya bioanuwai ya bahari na pwani pamoja na kuunganisha mikakati ya kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi katika utekelezaji wa NBSAP.

Kwa NBSAP Accelerator Partnership, Tanzania imeeleza rasmi nia ya kujiunga na ushirikiano huo ili kunufaika na uwezeshaji wa utekelezaji nchini, kuunganishwa na wataalam na washirika wa maendeleo wenye uwezo wa kusaidia maeneo yenye mapungufu ya kitaalam na kifedha, pamoja na kubadilishana uzoefu na nchi nyingine zinazotekeleza NBSAP.

Aidha, Tanzania imeomba NBSAP Mainstreaming Initiative kusaidia kuingiza malengo ya bioanuwai katika sera na mipango ya sekta mbalimbali, ikiwemo kilimo, utalii na nishati; wakati Sekretarieti ya CBD imeombwa kuendelea kutoa mwongozo wa kitaalam katika kuoanisha mfumo wa kitaifa wa ufuatiliaji na viashiria vya KM-GBF, kujenga uwezo wa kitaalam katika utoaji taarifa na kuhakikisha vipaumbele vya Tanzania vinazingatiwa katika programu za kikanda za kujenga uwezo.

Katibu Mkuu amesisitiza dhamira ya Serikali ya kuendelea kuhamasisha rasilimali za ndani na kuimarisha uratibu wa kitaifa, huku akitoa wito kwa washirika hao kushirikiana na Tanzania kuweka mpango mahsusi wa utekelezaji wenye ahadi za msaada wa kitaalam na kifedha kwa kipindi cha miezi 12 ijayo, hatua za Tanzania kushiriki katika NBSAP Accelerator Partnership, pamoja na kubainisha maeneo ya matokeo ya haraka yatakayotekelezwa ndani ya miezi sita.

Kwa umoja wao, wadau wote wameonesha utayari na kuahidi kuanza na kipaumbele cha kujenga uwezo wa kitaalam katika kufikia malengo ya utekelezaji wa NBSAP. Kwa kuanza watatoa fursa ya vijana kujengewa uwezo kuhusu Mkataba wa CBD na Itifaki zake.