Dodoma. Kampuni ya mawasiliano ya Yas imewahimiza wakulima kutumia huduma za kidijitali kupata taarifa za masoko, hali ya hewa na fursa za biashara, ikiwa ni njia ya kuongeza tija na kurahisisha shughuli zao za kilimo.
Akizungumza wakati wa Maonesho ya Nanenane yanayoendelea jijini Dodoma, Kaimu Mkuu wa Yas Kanda ya Kati, Richard Mmari, amesema kupanuka kwa huduma za mawasiliano nchini kunatoa fursa kwa wakulima kutumia teknolojia kufanya maamuzi sahihi kuanzia shambani hadi sokoni.
Amesema Yas imewekeza katika zaidi ya minara 4,900 ya 4G na 5G nchini, hatua ambayo imewezesha huduma za mawasiliano kuwafikia Watanzania wengi katika maeneo mbalimbali, ikiwemo vijijini ambako shughuli nyingi za kilimo zinafanyika.
“Leo mkulima anaweza kutumia simu kupata taarifa za bei za mazao, kufuatilia hali ya hewa na kutafuta masoko akiwa shambani au nyumbani. Hizi ni fursa ambazo zinaweza kumsaidia kupanga vizuri shughuli zake na kuongeza tija,” amesema Mmari.
Amesema pamoja na kupanua mtandao, Yas inaendelea kurahisisha upatikanaji wa simu janja kupitia mpango wa malipo ya awamu, ili kuwapa Watanzania wengi zaidi nafasi ya kutumia huduma zinazopatikana kidijitali.
Kwa mujibu wa Mmari, wakulima wanaotembelea Maonesho ya Nanenane jijini Dodoma wanaweza kufika katika banda la Yas kupata maelezo kuhusu mpango huo pamoja na huduma nyingine zinazoweza kuwasaidia katika shughuli zao za kila siku.
Yas itaendelea kuboresha huduma zake, hususan maeneo ya vijijini, ili wakulima na wananchi wengine waweze kushiriki kikamilifu katika uchumi wa kidijitali.

