Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, ametembelea pia Banda la Betaren Tanzania Limited, Kampuni Tanzu ya Schelokovo Agrohim ya Urusi inayojihusisha na uzalishaji wa mbolea, mbegu bora za mbogamboga na viuatilifu, wakati wa kilele cha Maonesho ya Kimataifa ya Kilimo ya Nanenane yaliyofanyika katika Viwanja vya Dkt. John Malecela, Nzuguni, jijini Dodoma, tarehe 8 Agosti 2026.

 

Bi. Tatiana Zubkova kutoka Schelokovo Agrohim amesema kampuni hiyo inatarajia kuleta na kusajili mbolea nyingine 13 mwezi Novemba 2026, pamoja na mbegu mbalimbali na viuatilifu. Ameongeza kuwa ushiriki wao katika maonesho hayo unalenga kujitambulisha kwa wadau, kutangaza bidhaa zao na kutoa elimu kuhusu teknolojia mpya wanazotarajia kuleta nchini.

 

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Udhibiti wa Mbolea Tanzania (TFRA), Bw. Joel Laurent, amesema kuwa ziara ya Mhe. Rais nchini Urusi tarehe 8 Juni 2026 ilichochea kampuni hiyo kuingia rasmi katika soko la Tanzania na kuanza taratibu za usajili wa bidhaa zake. Kwa sasa, kampuni hiyo imewasilisha bidhaa mbalimbali kwa ajili ya usajili, zikiwemo mbolea aina tatu; Ultramag Phosphorus Super ambayo tayari imesajiliwa kwa Namba ya Usajili FERT/11-2424, huku Ultramag Combi Oil Seeds na Ultramag Boron zikiwa katika hatua za kukamilisha usajili.

Sikukuu ya Wakulima Nanenane 2026 yanaongozwa na kaulimbiu: “Tambua Soko; Ongeza Tija Kutekeleza Dira 2050.”