Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mhe. Dkt. Hussein Ali Mwinyi, amesema elimu, maarifa na ubunifu havitakuwa na maana kamili iwapo havitatumika kutatua changamoto za jamii, kubadilisha maisha ya watu na kujenga mataifa yenye maendeleo endelevu, hivyo amewataka wahitimu wa Taasisi ya Teknolojia ya India Madras (IIT Madras), kuwa wabunifu na viongozi wa mabadiliko katika jamii zao.
Rais Dkt. Mwinyi ameyasema hayo leo, tarehe 17 Julai 2026, akiwa Mgeni Rasmi katika Mahafali ya 63 ya Taasisi ya Teknolojia ya India Madras (IIT Madras), yaliyofanyika jijini Chennai, nchini India.
Amesema elimu haipaswi kuonekana kuwa maandalizi ya kupata ajira pekee, bali ni nyenzo ya kujenga Taifa, kuimarisha jamii na kuandaa kizazi chenye maarifa, ujasiri na dhamira ya kuleta mabadiliko chanya.
Ameeleza kuwa mafanikio ya kweli hayapimwi kwa ukubwa wa cheo, nafasi ya kazi, utajiri au kutambuliwa binafsi, bali kwa maisha yaliyoguswa na kuboreshwa, fursa zilizofunguliwa kwa wengine, imani iliyojengwa na matumaini yaliyoachwa katika jamii.
Rais Dkt. Mwinyi amewahimiza wahitimu kuzingatia uadilifu, unyenyekevu, huruma na utumishi kwa watu, akisisitiza kuwa ubunifu haupaswi kupimwa kwa ugumu wa teknolojia, bali kwa uwezo wake wa kuleta manufaa kwa wananchi.
Aidha, amesema Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imeweka elimu katika kiini cha Dira ya Maendeleo ya Taifa, ikiwa msingi wa ubunifu, ustawi wa wananchi, utawala bora na utekelezaji wa Ajenda ya Uchumi wa Buluu. Ameongeza kuwa maendeleo ya kweli yanahitaji uwekezaji katika watu, hususan kuwawezesha vijana kuwa wazalishaji wa maarifa na teknolojia.
Akizungumzia Kampasi ya IIT Madras Zanzibar, Rais Dkt. Mwinyi amesema kuanzishwa kwake kumefungua ukurasa mpya wa ushirikiano wa kielimu baina ya Tanzania na India, pamoja na kutoa fursa za kubadilishana maarifa, uzoefu na tamaduni baina ya wanafunzi wa Afrika na India.
Amesema dhamira ya Zanzibar ni kuifanya kampasi hiyo kuwa kituo cha umahiri katika elimu, utafiti, ubunifu na ujasiriamali kwa ukanda wa Afrika Mashariki, itakachowakutanisha wataalamu kutafuta suluhisho za changamoto na kuibua fursa mpya za maendeleo.
Rais Dkt. Mwinyi pia ameipongeza IIT Madras kwa mchango wake katika kuzalisha wahandisi, wanasayansi na wajasiriamali, pamoja na kuendeleza tafiti na ubunifu wenye mchango katika maendeleo ya jamii na uchumi duniani.
Katika hafla hiyo, Rais Dkt. Mwinyi ameshiriki kuwatunuku wahitimu wa ngazi mbalimbali za elimu ya juu, wakiwemo wa shahada ya kwanza na shahada ya uzamivu (PhD). Aidha, amekabidhiwa Tuzo Maalum na uongozi wa IIT Madras kwa kutambua mchango wake katika kuanzishwa na kuendelezwa kwa Kampasi ya IIT Madras Zanzibar. Hafla hiyo pia iliambatana na uzinduzi wa mradi wa ujenzi wa kampasi mpya ya kudumu ya IIT Madras Zanzibar.
Mahafali hayo yalihudhuriwa na Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar, Mhe. Lela Mohamed Mussa; Mkurugenzi wa IIT Madras, Profesa V. Kamakoti; Balozi wa Tanzania nchini India, Mhe. Anisa Kapufi Mbega; Balozi wa India nchini Tanzania, Mhe. Bishwadip Dey; pamoja na viongozi mbalimbali, wahadhiri, wazazi na familia za wahitimu.
Rais Dkt. Mwinyi aliondoka Zanzibar tarehe 16 Julai 2026, akiambatana na Mkewe, Mhe. Mama Mariam Mwinyi, na ujumbe wake, kuelekea nchini India kwa ziara ya kikazi, ambapo alipowasili jijini Chennai alipokelewa na Balozi wa Tanzania nchini India, Mhe. Anisa Kapufi Mbega; Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Dkt. Ngwaru Maghembe (Mb.); pamoja na viongozi mbalimbali wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya India.

