Mkutano wa 28 wa Kamati ya Mawaziri wa Asasi ya Siasa, Ulinzi na Usalama ya Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) umehitimishwa leo Julai 18, 2026 mjini Salima, Malawi, huku nchi zikihimizwa kutekeleza yaliyoafikiwa katika mkutano huo ambayo yanalenga kuimarisha amani, ulinzi na usalama kwenye kanda ya SADC. 

Tanzania ikiwa ni moja ya nchi waasisi wa SADC, ilishiriki mkutano huo uliofanyika katika ngazi ya Makatibu Wakuu Jula 13 na 14, 2026 na ngazi ya Mawaziri Julai 16 na 17, 2026.

Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki (EAC), Mhe. James Millya akiambatana na Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mhe. Ayoub Mohammed Mahmoud walishiriki katika ngazi ya Mawaziri na Naibu Katibu Mkuu, Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Said Shaib Mussa na Naibu Katibu Mkuu, Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi, Dkt. Maduhu Kazi wao walishiriki ngazi ya Makatibu Wakuu. 

Ushiriki wa Tanzania ambao ulihusisha pia wawakilishi kutoka vyombo vya ulinzi na usalama nchini ni ishara ya wazi kuwa suala la ulinzi na usalama linapewa umuhimu wa kipekee, sio nchini tu bali katika kanda nzima ya SADC na kwamba jambo hilo linahitaji umoja wa nchi wanachama ili liweze kuimarishwa kikamilifu.