Dar es Salaam

Mradi wa ufufuaji wa Reli ya Tanzania na Zambia (TAZARA) umefikia hatua muhimu baada ya Shirika la China Civil Engineering Construction Corporation (CCECC), kampuni tanzu ya China Railway Construction Corporation (CRCC), kuzindua rasmi ujenzi wa Kituo kipya cha Mafunzo cha TAZARA pamoja na Kituo cha Kisasa cha Udhibiti wa Uendeshaji.

Hafla ya uwekaji wa jiwe la msingi imefanyika leo jijini Dar es Salaam na kuhudhuriwa na Katibu Mkuu wa Wizara ya Uchukuzi, Prof. Godius Kahyarara, Mwenyekiti wa CCECC, Bw. Li Chongyang, Balozi wa Jamhuri ya Watu wa China nchini Tanzania, Mhe. Chen Mingjian, pamoja na Mkurugenzi Mtendaji na Afisa Mtendaji Mkuu wa TAZARA, Mhandisi Bruno Ching’andu.

Kituo kipya cha Mafunzo kitajengwa katika eneo lenye ukubwa wa mita za mraba 21,800, huku majengo yake yakichukua eneo la sakafu la mita za mraba 9,641. Kituo hicho kitakuwa na maabara za mafunzo, madarasa ya nadharia, maeneo ya kazi za ofisi na vyumba vya mikutano vya ukubwa mbalimbali.

Aidha, kituo hicho kinatarajiwa kuwa nguzo muhimu katika kuimarisha ujuzi wa kitaalamu wa watumishi wa reli na kuhakikisha upatikanaji endelevu wa wataalamu wenye sifa watakaosimamia hatua za ufufuaji, uendeshaji wa kila siku na maendeleo ya muda mrefu ya TAZARA.

Sambamba na hilo, Kituo cha Kisasa cha Udhibiti wa Uendeshaji kitakuwa kitovu kikuu cha kuratibu na kusimamia shughuli zote za reli. Kituo hicho kitawekewa mifumo ya kisasa ya mawasiliano ya uongozaji wa treni, skrini kubwa za kuonesha taarifa, mifumo jumuishi ya ufuatiliaji, majukwaa ya usimamizi wa taarifa pamoja na vifaa vingine muhimu vya kiteknolojia.

Mara kitakapokamilika, kituo hicho kitawezesha uratibu wa pamoja wa mienendo ya treni, upangaji wa uwezo wa usafirishaji na utekelezaji wa mipango ya uendeshaji katika mtandao mzima wa Reli ya TAZARA.

Ujenzi wa vituo hivyo viwili unaonekana kuwa hatua muhimu katika utekelezaji wa mpango wa kuifufua TAZARA, ukilenga kuibadilisha reli hiyo kuwa ya kisasa, yenye ufanisi, salama na endelevu ili kuongeza mchango wake katika uchumi wa Tanzania, Zambia na ukanda wa Afrika Mashariki na Kusini.