Na John Bukuku, Dar es Salaam

Julai 1, 2026 – Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Yusuf Mwenda, amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa kutoa kibali cha kuanzishwa kwa timu ya soka ya TRA United Sports Club ambayo imeonesha mafanikio makubwa katika msimu wake wa kwanza wa kushiriki Ligi Kuu Tanzania.

Mwenda ametoa kauli hiyo leo katika hafla ya utoaji wa Tuzo ya Rais kwa Mlipakodi Bora pamoja na maadhimisho ya miaka 30 ya TRA iliyofanyika katika ukumbi wa Milimani City jijini Dar es Salaam, ambapo amesema uamuzi wa Rais kuruhusu kuanzishwa kwa timu hiyo umeleta matokeo chanya.

Amesema TRA ilipoanzisha mpango wa kuwa na timu ya soka iliomba ushauri na kibali kutoka kwa Rais Samia, ambaye aliridhia na kutoa ruhusa, hatua ambayo imewezesha taasisi hiyo kushiriki kikamilifu katika kukuza michezo nchini.

“Mheshimiwa Rais, wakati tunaanzisha timu hii tuliomba ushauri wako na kibali chako, hukusita kuridhia na ulituruhusu kuwa na timu. Leo tunayo timu inayoitwa TRA United Sports Club,” amesema Mwenda.

Ameeleza kuwa TRA United imefanya vizuri kwa mwaka wake wa kwanza katika Ligi Kuu Tanzania baada ya kumaliza msimu ikiwa nafasi ya tano kati ya timu 16 zilizoshiriki ligi hiyo, jambo alilolitaja kuwa ni mafanikio makubwa kwa timu changa.

Mwenda amesema mafanikio hayo yanaonesha kuwa michezo ni sehemu muhimu ya kujenga mahusiano bora, kuimarisha ushirikiano na kufikisha ujumbe kwa jamii kuhusu umuhimu wa kulipa kodi kwa hiari.

Aidha, amewapongeza wachezaji, benchi la ufundi na uongozi wa TRA United kwa kujituma na kuiwakilisha vyema taasisi hiyo katika ushindani wa Ligi Kuu Tanzania.

Amesema TRA itaendelea kuunga mkono maendeleo ya timu hiyo ili iweze kukua zaidi na kuwa sehemu ya mafanikio ya taasisi hiyo katika sekta ya michezo nchini.

TRA United Sports Club imekuwa miongoni mwa miradi ya TRA inayolenga kutumia michezo kama jukwaa la kujenga mahusiano na jamii, huku mafanikio ya msimu wake wa kwanza yakionekana kuwa hatua muhimu katika historia ya timu hiyo.