Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan akitoa Tuzo ya Rais kwawalipakodi kwenye Maadhimisho ya miaka 30 ya Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) katika ukumbi wa Mlimani City Jijini Dar es Salaam, tarehe 01 Julai, 2026.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan akizungumza jambo na mmoja wa wafanyabiashara ambaye ni mlemavu katika Maadhimisho ya miaka 30 ya Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) baada ya kuwasili katika ukumbi wa Mlimani City Jijini Dar es Salaam, tarehe 01 Julai, 2026.

………….. 

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, amesema zawadi kubwa atakayoipata baada ya kumaliza muda wake wa uongozi ni kuona Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) ikiwa taasisi imara, yenye weledi na inayokusanya kodi kwa uadilifu kwa ajili ya kujenga taifa linalojitegemea.

Rais Samia aliyasema hayo Julai 1, 2026 wakati wa hafla ya utoaji wa Tuzo za Rais kwa Walipakodi Bora pamoja na maadhimisho ya miaka 30 ya kuanzishwa kwa TRA iliyofanyika katika ukumbi wa Mlimani City jijini Dar es Salaam.

Alisema mafanikio ya TRA katika kipindi cha miaka 30 yameonyesha uwezo wa Tanzania kujenga mfumo wa ndani wa ukusanyaji wa mapato, huku akisisitiza kuwa mamlaka hiyo inapaswa kuendelea kukusanya kodi kwa haki bila kuwadhulumu wafanyabiashara.

“Imani huzaa imani, TRA ikijenga imani na kumhudumia mlipa kodi kwa haki, heshima na weledi itajenga imani ya walipa kodi kwa TRA na Serikali,” alisema Rais Samia.

Alisema ulipaji kodi ni uzalendo na ushujaa kwa maendeleo ya taifa, lakini akasisitiza kuwa wajibu huo unapaswa kwenda sambamba na mamlaka ya kodi kuhakikisha inakusanya kwa uadilifu na Serikali kutumia mapato hayo kwa manufaa ya wananchi.

Rais Samia alisema Serikali itaendelea kuboresha mazingira ya biashara, kukuza biashara ndogo na za kati pamoja na kuimarisha mifumo ya kodi ili iwe rahisi, ya kisasa na inayozingatia haki.

Kwa upande wake, Waziri wa Fedha, Balozi Khamis Mussa Omar, alisema miaka 30 ya TRA ni ushahidi wa safari ya mageuzi ya kujenga uwezo wa taifa katika kusimamia mapato ya ndani.

Alisema kuanzishwa kwa TRA kulitokana na hatua za Serikali za kuboresha usimamizi wa kodi, ambapo taasisi hiyo imeendelea kuwa nguzo muhimu katika kugharamia huduma za jamii na miradi ya maendeleo.

Balozi Omar alisema mfumo wa kodi unatakiwa kuendelea kubadilika kulingana na ukuaji wa uchumi na mazingira ya biashara ili kuongeza ufanisi na kupanua wigo wa walipakodi nchini.

Naye Kamishna Mkuu wa TRA, Yusuf Mwenda, alimshukuru Rais Samia kwa kukubali kuwa mgeni rasmi katika hafla hiyo na kwa kubadilisha hadhi ya tuzo hizo kuwa Tuzo za Rais kwa Walipakodi Bora.

Alisema mabadiliko hayo ni ishara ya kutambua mchango wa walipakodi katika maendeleo ya taifa.
Kamishna Mwenda alisema katika kipindi cha mwaka wa fedha 2025/2026 TRA imekusanya shilingi trilioni 37.957 kati ya lengo la trilioni 36.66, sawa na ufanisi wa asilimia 103.4.

Alisema mafanikio hayo yamepatikana kutokana na ushirikiano kati ya TRA na walipakodi, huku akieleza kuwa mamlaka hiyo itaendelea kuboresha mifumo ya teknolojia, kupanua wigo wa walipakodi na kuwezesha mazingira rafiki ya biashara.