NA NOEL RUKANUGA, DAR ES SALAAM
Simba SC imeendelea kuonyesha ubabe wake nyumbani baada ya kuichapa Tanzania Prisons mabao 4-0 katika mchezo wa Ligi Kuu uliopigwa Uwanja wa KMC Complex, huku kiungo mahiri Clatous Chama akiendelea kuwa nguzo muhimu ya ushindi wa Wekundu wa Msimbazi.
Ushindi huo unakuwa wa 14 kwa Simba msimu huu katika mechi 22 walizocheza, huku wakizidi kujikita nafasi ya pili kwenye msimamo wa ligi kwa kufikisha pointi 49 na kuendelea kuisogelea Young Africans SC iliyo kileleni ikiwa na pointi 54.
Simba ilianza mchezo kwa kasi na kupata nafasi ya kuandika bao la mapema dakika ya 12 baada ya kupewa penalti, lakini mshambuliaji Seleman Mwalimu akashindwa kuitumia vizuri baada ya kupiga mpira uliopaa juu ya lango.
Hata hivyo, wenyeji walifanikiwa kuvunja ukuta wa Prisons dakika ya 27 kupitia kiungo Morrice Abraham aliyemalizia mpira uliotemwa na mabeki wa Prisons. Hilo likiwa bao lake la pili msimu huu akiwa na jezi ya Simba, sambamba na asisti moja aliyotoa hadi sasa.
Dakika chache baadaye, Chama akaendeleza kiwango chake bora kwa kufunga bao maridadi baada ya kumchambua kipa Mussa Mbisa kwa mpira wa juu uliowaacha mashabiki wakishangilia kwa nguvu.
Kabla ya mapumziko, Seleman Mwalimu akajisahihisha kwa kufunga bao la tatu akiunganisha pasi safi ya Libase Gueye, na kuipeleka Simba mapumzikoni ikiwa mbele kwa mabao 3-0.
Kipindi cha pili Simba iliendelea kushambulia kwa kasi, ambapo dakika ya 62 beki Ismael Toure alifunga bao la nne kwa kichwa akimalizia kona iliyopigwa na Chama.
Chama sasa ameendeleza moto wake kwa kufunga katika mechi tatu mfululizo baada ya kuzifumania nyavu timu za Yanga, JKT Tanzania na Tanzania Prisons, akionyesha kuwa katika kiwango bora kwa sasa.
Kwa upande wa Prisons, walionekana kuzidiwa kwa kiasi kikubwa katika mchezo huo, huku kipa Mbisa akiwa tegemeo lao kubwa kwa kuokoa mashambulizi kadhaa hatari kutoka kwa safu ya ushambuliaji ya Simba.
Baada ya kipigo hicho, Tanzania Prisons imeendelea kubaki nafasi ya 15 kwenye msimamo wa ligi ikiwa na pointi 14 baada ya kucheza mechi 22, na sasa inakabiliwa na presha kubwa ya kupambana kujinasua kwenye hatari ya kushuka daraja.
