Mabao  mawili ya dakika ya 18 na 63 ya kiungo nyota wa Yanga, Allan Okello, sambamba na lile la dakika ya 75 kutoka kwa Maxi Nzengeli, yametosha kuipa timu hiyo pointi tatu dhidi ya Coastal Union, katika mechi ya Ligi Kuu Bara iliyopigwa Leo Mei 9, 2026 kwenye Uwanja wa KMC Complex, Mwenge, Dar es Salaam.

Bao la kwanza Okello alilifunga baada ya kupokea pasi ya Prince Dube na kufanya kwenda mapumziko Yanga ikiwa mbele kwa bao 1-0.

Kipindi cha pili pasi ya Pacome Zouzoua ikamkuta Okello akiwa nje kidogo ya boksi, akaachia shuti lililomshinda kipa wa Coastal Union, Chuma Ramadhan na kujaa wavuni.

Baadaye Okello akamuwekea pasi nzuri Maxi aliyehitimisha ushindi huo na kumfanya Okello sasa kufikisha mabao matano na asisti saba.

Ushindi huo kwa Yanga wa mabao 3-0, ni wa kwanza kwa Kaimu Kocha Mkuu, Abdihamid Moallin ‘Master Lecturer’, tangu alipoteuliwa kukiongoza hicho hicho Mei 6, 2026, akichukua nafasi ya Mreno, Pedro Goncalves.

Uongozi wa Yanga ulitangaza kuachana na Pedro, ikiwa ni muda mfupi tangu timu hiyo ishinde bao 1-0 dhidi ya KMC FC katika mechi ya Ligi Kuu Bara, akidumu ndani ya kikosi hicho kwa siku 193, tangu alipotambulishwa rasmi, Oktoba 25, 2025.

Ushindi wa leo kwa Yanga unaifanya kuendeleza kijikita kileleni mwa msimamo na pointi 54, baada ya kucheza mechi 22 za Ligi Kuu hadi sasa.

Kwa upande wa Coastal Union, hii ni mechi ya pili mfululizo kupoteza, baada ya Mei 5, 2026, kuchapwa mabao 3-2, ugenini dhidi ya Fountain Gate.

Pia kichapo hicho kwa Coastal Union ni cha pili kwa kocha mkuu wa timu hiyo, Fikiri Elias, tangu alipoteuliwa Aprili 10, 2026, akichukua nafasi ya Mohamed Muya aliyeondoka Aprili 8, 2026.