Na.Sophia Kingimali.

Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) limefunga rasmi Mashindano ya Kombe la CNS Cup 2026 katika Kambi ya JKT Mgulani jijini Dar es Salaam, huku likisisitiza umuhimu wa michezo katika kuimarisha nidhamu, uzalendo, afya na kuibua vipaji vya vijana wanaojitolea kulitumikia taifa kupitia jeshi hilo.

Akifunga mashindano hayo kwa niaba ya Mkuu wa JKT, Meja Jenerali Rajabu Mabele, Mkuu wa Taasisi ya Mafunzo JKT, Brigedia Jenerali Peter Mnyani,amesema michezo imeendelea kuwa sehemu muhimu ya mafunzo ya JKT kwa kuwa inajenga uwezo wa kimwili na kiakili, huku ikiwajengea vijana nidhamu, moyo wa kujituma, uongozi na mshikamano unaohitajika katika utendaji wa majukumu ya kijeshi.

Amesema mashindano ya CNS Cup yameendelea kuwa jukwaa muhimu la kutambua na kuendeleza vipaji vya wanamichezo kutoka vikosi mbalimbali vya JKT, ambao baadaye hujiunga na timu teule za jeshi hilo kushiriki mashindano ya kijeshi na kitaifa.

“Michezo ni ajira na ni fursa ya maendeleo kwa vijana. Wale waliopata nafasi ya kuchaguliwa wanapaswa kuendelea kufanya mazoezi kwa bidii na kulinda vipaji vyao kwa manufaa ya JKT na taifa kwa ujumla,” amesema.

Aidha, amewahimiza washiriki ambao hawakufanikiwa kuchaguliwa kutokata tamaa, bali waendelee kujiendeleza kwa kuwa nafasi za kuwakilisha JKT katika mashindano mbalimbali bado zipo.

Brigedia Mnyani amesema JKT tayari limeanza maandalizi ya mashindano yajayo ya KDF Cup na BAMATA, akieleza kuwa lengo ni kurejesha ushindani mkubwa na kufanya vizuri zaidi kuliko ilivyokuwa katika mashindano yaliyopita.

Aidha Brigedia Jenerali Mnyani amewapongeza makamanda, walimu, viongozi na washiriki wote kwa kuonyesha nidhamu ya hali ya juu, ushindani wa haki na uvumilivu katika kipindi chote cha mashindano hayo.

Kwa upande wake, Kamanda wa Kikosi cha JKT Mgulani, Kanali Ernest Sambila, amesema michuano hiyo ilianza katika ngazi za vikosi kabla ya kuendelea katika kanda tano za JKT nchini, ambapo wanamichezo walishindana katika michezo mbalimbali ikiwemo mpira wa miguu, mpira wa pete, mpira wa kikapu na mingineyo.

Naye Mkurugenzi wa Elimu, Sanaa na Utamaduni JKT, Kanali Amos Mollo, amesema mashindano hayo yamewezesha kupatikana kwa wanamichezo wenye vipaji watakaojiunga na timu za JKT kwa ajili ya kushiriki mashindano ya majeshi na yale ya kitaifa.

Amesema zaidi ya wanamichezo 1,600 walishiriki katika hatua mbalimbali za mashindano hayo, huku mchakato wa uteuzi ukizingatia uwezo, nidhamu na utayari wa kushiriki katika timu za jeshi.

Kanali Mollo amebainisha kuwa michezo imeendelea kuwa nyenzo muhimu ya kujenga umoja, kuimarisha afya na kuibua vipaji vya vijana, sambamba na kuandaa kizazi chenye uwezo wa kushiriki katika maendeleo ya taifa.

Sambamba na hayo Brigedia Jenerali Mnyani aliwataka vijana wanaorejea katika vikosi vyao kuendelea kuheshimu maadili, mila na taratibu za kijeshi walizojifunza, kabla ya kutangaza rasmi kufungwa kwa Mashindano ya Kombe la Mkuu wa JKT 2026 yaliyohitimishwa Juni 23, 2026 katika Kambi ya JKT Mgulani, Dar es Salaam.