Na Mwamvua Mwinyi, Pwani
VIJANA 100 kati ya 7,852 waliojitokeza kushiriki mashindano ya Vijana Uchumi Challenge 2025/2026 wameingia kambini katika Shule ya Uongozi ya Mwalimu Nyerere, Kwa Mfipa, Kibaha mkoani Pwani kuwania kitita cha Sh milioni 50 kwa mshindi wa kwanza.
Washiriki hao watakuwa kambini kwa siku tatu hadi Juni 27, 2026, wakipatiwa mafunzo na kufanya tathmini ya mawazo yao kabla ya kufanyika mchujo utakaobakiza washiriki 30 na baadaye 10 bora watakaofika hatua ya mwisho.
Akizindua kambi hiyo, Naibu Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais (Maendeleo ya Vijana), Dkt. Kedmon Elisha Mapana, alisema washindi 10 bora watapatikana Julai 6, 2026 ambapo mshindi wa kwanza atapata Sh milioni 50, wa pili Sh milioni 30 na wa tatu Sh milioni 20, huku washiriki saba wengine wakipata kifuta jasho cha Sh milioni tatu kila mmoja.
Alisema mawazo yaliyowasilishwa yalipaswa kuzingatia vigezo saba ambavyo ni ubunifu, uelewa wa changamoto za kiuchumi, uhalisia wa utekelezaji, mchango katika kukuza uchumi wa taifa, uwezo wa kuleta fursa, uendelevu na ubora wa uwasilishaji.
Dkt. Mapana alisema mawazo mengi ya washiriki yamejikita katika TEHAMA na huduma za kidijitali kwa asilimia 30.7, kilimo na teknolojia asilimia 27.8, viwanda na uzalishaji asilimia 21, nishati asilimia 5.8 na usafirishaji asilimia moja.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Kamati ya Kitaifa ya Uchumi Challenge, Joseph Malekela, alisema mashindano hayo yalizinduliwa Aprili 10, 2026 na baada ya mchakato wa uchambuzi wa mawazo ya vijana zaidi ya 7,000 waliomba kushiriki, hatimaye washiriki 100 walifanikiwa kufikia hatua ya kambi.
Alisema washiriki hao wametoka Tanzania Bara na Zanzibar wakiwakilisha mikoa 27 nchini.
Naye Mwenyekiti wa Jopo la Majaji, Profesa Neema Mori, alisema majaji sita wenye uzoefu katika nyanja za uchumi, utafiti, siasa na kilimo wataangalia ubora wa mawazo kwa kuzingatia vigezo vilivyowekwa.
“Vijana wote 100 ni washindi kwa hatua waliyofikia, lakini tunahitaji kupata wale watakaokuwa na mawazo bora zaidi yenye mchango kwa taifa,” alisema Profesa Mori.
Mmoja wa washiriki, Adrian Sabudema (28) kutoka Shinyanga, aliishukuru Serikali ya Awamu ya Sita kupitia Ofisi ya Rais (Maendeleo ya Vijana) kwa kuanzisha mashindano hayo akisema yamefungua nafasi kwa vijana kuonyesha uwezo na mawazo yao ya ubunifu.
Mashindano ya Vijana Uchumi Challenge yalitambulishwa na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Maendeleo ya Vijana), Joel Arthur Nanauka, Aprili 10, 2026, Washindi kumi wanatarajiwa kutangazwa Julai 6, 2026 katika ukumbi wa Mikutano wa Julius Nyerere International Convention Centre (JNICC) mbele ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe.Dkt.Samia Suluhu Hassan anayetarajiwa kuwa Mgeni rasmi.

