WAZIRI MKUU Dkt. Mwigulu Nchemba amesema Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan amechochea kufanyika kwa mageuzi makubwa katika sekta ya michezo nchini.

Amesema hayo jana Jumamosi (Mei 9, 2026) alipomwakilisha Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mheshimiwa Dkt. Hussein Ali Mwinyi, katika hafla ya utoaji tuzo za michezo za Baraza la Michezo la Taifa (NSCA), zilizofanyika kwenye ukumbi wa The Super Dom, Masaki jijini Dar es Salaam.

Mheshimiwa Dkt. Mwigulu amesema Mheshimiwa Rais Samia amefanya mambo mengi yanayodhihirisha nia yake ya dhati ya kuendeleza michezo nchini.

“Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan amefanya mageuzi makubwa kwenye michezo, kuanzishwa kwa mfuko wa maendeleo ya michezo ni miongoni mwa mambo makubwa kwenye sekta ya michezo.” Amesema Waziri Mkuu Mwigulu.

Waziri Mkuu ameongeza kwa kusema kuwa “Goli la mama na knock out ya mama vimeongeza ari kwa wanamichezo na vilabu vyetu vya Tanzania, kama mlivyoona timu zetu zimefanya vizuri kwenye mashindano ya kimataifa, hii ni kutokana na chachu iliyoletwa na goli la mama.”

“Ninyi wenyewe ni mashuhuda, miaka ya nyuma timu zetu zilikuwa zikipangwa na timu za kaskazini na magharibi tulikuwa tunajua ni wasindikizaji tu, lakini kwa sasa, kibao kimegeuka, nchi yetu inafanya vizuri na inazungumzwa vizuri.” Amesisitiza Dkt. Mwigulu.

Pamoja na hayo, Waziri Mkuu amesema eneo lingine linalodhihirisha kuwa serikali inaipa michezo kipaumbele ni uwekezaji katika miundombinu, mathalani ujenzi wa uwanja wa AFCON Arusha na ukarabati mkubwa wa uwanja wa Benjamin Mkapa.

“Haya yote yataendelea kuweka chachu ya mafanikio katika sekta ya michezo nchini. Nikiwa Msimamizi Mkuu wa shughuli za Serikali, nitaendelea kusimamia vizuri maono haya ya Rais wetu ili yatoe matokeo yaliyokusudiwa.” Amesema Waziri Mkuu.

Akizungumzia tuzo hizo, Waziri Mkuu amesema ni motisha muhimu kwa wadau wa michezo nchini na sehemu ya mkakati wa kuimarisha maendeleo ya michezo na jukwaa muhimu la kuwatambua wanamichezo wanaoliwakilisha vyema Taifa, ndani na nje ya nchi.

Kutokana na umuhimu wanamichezo kutambuliwa vipaji vyao kuanzia kwenye umri mdogo, Waziri Mkuu ameitaka Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi kuhakikisha inalinda maeneo ya wazi yaliyotengwa kwa ajili ya michezo ili vijana wa Kitanzania wapate majukwaa ya kuonesha vipaji vyao.

Wadau mbalimbali wa michezo, wakiwemo wachezaji, wanahabari na viongozi wa michezo waliofanya vizuri kwa mwaka 2025 wametambuliwa na kupewa tuzo.