Na Baltazar Mashaka, Mwanza

UKOO wa Wasindi, mmoja wa koo za Wakerewe wilayani Ukerewe, umefungua ukurasa mpya wa umoja na maendeleo baada ya kufanya mkutano mkuu wa mwaka na kuchagua viongozi wapya watakaoongoza kwa kipindi cha mwaka mmoja.

Mkutano huo uliofanyika leo katika Kijiji cha Nanumi, Wilaya ya Ukerewe, ulijadili masuala mbalimbali ya kuimarisha mshikamano, kutatua changamoto za ukoo na kuweka mikakati ya maendeleo.

Akizungumza baada ya kuchaguliwa kuwa Mwenyekiti wa ukoo huo, Deus Lukanima Ngoroma alisema uongozi mpya umejipanga kurejesha mshikamano uliokuwa umedorora kwa miaka mingi kutokana na wanaukoo kushindwa kushirikiana katika shughuli mbalimbali.

Alisema hali hiyo ilifikia hatua ya baadhi ya wanaukoo kutosalimiwa na kushindwa hata kushirikiana katika shughuli za kijamii, jambo lililodhoofisha umoja wa ukoo.

“Tumekubali dhamana hii kwa moyo wa kujitolea na tutaongoza kwa haki, uwazi na usawa bila kumwonea mtu yeyote. Tunaomba wanaukoo wote watupatie ushirikiano ili kujenga ukoo imara wenye mshikamano na maendeleo,” alisema.

Ngoroma alisema viongozi hao watawahudumia wanaukoo wote bila ubaguzi, huku akiwasihi kutowadharau kutokana na umri wao mdogo bali kuwapa ushirikiano ili kutimiza malengo yaliyowekwa.

Katibu Mkuu mpya wa ukoo huo, Gatahwa Kilangi, aliwataka wanaukoo kuheshimu viongozi wao na kutekeleza maelekezo yanayotolewa kwa lengo la kuimarisha nidhamu, umoja na maendeleo.

“Ni vigumu kumwongoza mtu anayepuuza maelekezo ya viongozi. Tunapokumbushana tunafanya hivyo kwa manufaa ya ukoo. Tuwaheshimu viongozi wetu na kuthamini muda na rasilimali wanazotumia kututumikia,” alisema.

Katibu Msaidizi, Mnaku Ngoroma, alisema amepokea jukumu hilo kwa unyenyekevu na kuahidi kushirikiana na viongozi wenzake kuhakikisha ukoo unakuwa mfano wa umoja na maendeleo.

Aliwaomba wanaukoo kuendelea kutoa ushauri na ushirikiano pale uongozi utakapohitaji ili kuimarisha utendaji na kufanikisha malengo ya pamoja.

Akitoa ushauri kwa uongozi mpya, Mhazini mstaafu wa ukoo huo, Baltazar Mashaka, alisema viongozi wanapaswa kuongoza kwa weledi, kubuni mikakati ya maendeleo, kuhimiza uwajibikaji na kujenga utamaduni wa kuweka akiba kwa ajili ya shughuli za maendeleo ya ukoo.

Kwa upande wake, Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Maadili, Joseph Mkono, aliwataka wanaukoo kuendeleza ushirikiano ili kuimarisha maendeleo ya ukoo.

Naye Mjumbe wa Kamati ya Maadili, Lusato Julius Bakarazya, aliwataka wanaukoo kusameheana na kuacha tofauti zilizopita, akisema msamaha, maridhiano na umoja ni nguzo muhimu za maendeleo endelevu ya ukoo wa Wasindi.