Na Mwandishi wetu, BabatiĀ
NAIBU Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Regina Ndege ameshiriki kufunga mkutano mkubwa wa Injili mji mdogo wa Gallapo Wilayani Babati Mkoani Manyara, kwa kuwaasa waumini na viongozi wa dini kuombea amani Taifa na kumuombea afya njema Rais Samia Suluhu Hassan ili aweze kuendelea kuingoza vyema Tanzania.
Naibu Waziri Ndege ambaye pia ni Mbunge wa Viti maalum wa Mkoa wa Manyara, ameeleza hayo wakati akifunga mkutano mkubwa wa injili ulioandaliwa na Kanisa la Tanzania Assemblies of God (TAG) Gallapo.
Ameliomba Kanisa kuendelea kuiombea nchi iwe na amani na utulivu pamoja na kumuombea Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt Samia Suluhu Hassan afya njema.
“Ili tuweze kuishi vyema kwa kufanya maendeleo na kuwa na amani kwenye familia na nchi kwa ujumla tunapaswa kuendelea kuomba kwa Mungu atujalie amani na utulivu na pia kumuombea afya njema kiongozi wetu anayeongoza nchi,” amesema Naibu Waziri Ndege.
Amewapongeza viongozi wa dini kwa kuendelea kuwa na jukumu la kuiombea nchi na viongozi wake sambamba na kuwaomba waumini kutenda matendo mema ya kumpendeza Mungu.
Mkutano huo umehusisha umoja wa makanisa yote ya Kipentekoste Wilayani Babati na umehitimishwa katika eneo la viwanja vya mpira Gallapo.
Mchungaji wa TAG Gallapo, Steven Konki amemshukuru Naibu Waziri Ndege kwa kutenga muda wake na kuhudhuria kwenye mkutano huo wa Injili.
“Tunakushukuru kwa kuja kwani upendo wako kwetu ni mkubwa na kila wakati umekuwa baraka kwetu, tunaendelea kukuombea afya njema, kuombea amani ya Taifa letu na kumuombea afya njema Rais wetu Dkt Samia ili azidi kutuongoza vyema,” amesema Mchungaji Konki.
