Na Mwandishi wetu, Mirerani
Washabiki na wapenzi wa timu ya Simba, Tawi la Tanzanite mji mdogo wa Mirerani wilayani Simanjiro mkoani Manyara, wanatarajia kushiriki tamasha la wiki ya Simba kwa kufanya mambo mbalimbali ya kijamii ikiwemo kuchangia damu kwenye kituo cha afya Mirerani.
Mwenyekiti wa Tawi la Simba Tanzanite, Mohamed Said akizungumza mji mdogo wa Mirerani Agosti 3, 2026 amesema wana Simba watashiriki wiki ya Simba kwa kukimbia mbio fupi hadi kituo cha afya Mirerani na kuchangia utoaji wa damu.
Mwenyekiti Said amewaalika wana Simba wote wa mji mdogo wa Mirerani na mkoa wa Manyara kwa ujumla kushiriki tamasha la wiki ya Simba ili kufanikisha tukio hilo.
“Tunawaomba wana Simba wajitokeze kwa wingi siku ya Ijumaa Agosti 7, 2026 wakiwa na sare za jezi za Simba mpya na za zamani ili kufanikisha wiki ya Simba hapa mji mdogo wa Mirerani ikiwemo kutembea kituo cha watoto yatima,’ amesema.
Katibu wa Tawi la Simba Tanzanite Mirerani, David Azaria amesema wanaendelea kuandikisha majina ya wanachama wenye sifa ili waongeze idadi ya wanachama wao.
Azaria amesema Tawi la Simba Tanzanite Mirerani wanatangaza utalii wa ndani ikiwemo madini ya Tanzanite ambayo kwa hapa duniani yanapatikana Tanzania, mkoa wa Manyara wilaya ya Simanjiro, mji mdogo wa Mirerani pekee.
