Mkuu wa Wilaya ya Ngorongoro,Brigedia Jenerali Wilson Sakulo akizungumza mara baada ya kutembelea banda hilo
Afisa Mahusiano kutoka kampuni hiyo ,Lee Mamasita akizungumza na waandishi wa habari jijini Arusha
Happy Lazaro,Arusha .
Arusha .Mkuu wa Wilaya ya Ngorongoro,Brigedia Jenerali Wilson Sakulo amepongeza uongozi wa kampuni ya West Kilimanjaro Ranching kwa kuendelea kutoa elimu ya matumizi bora ya mbegu za kisasa za mifugo ambazo zinawawezesha wafugaji kubadili mbinu za uzalishaji.
Ameyasema hayo leo wakati akizungumza katika banda hilo katika maonesho ya nanenane Themi Njiro mara baada ya kujionea namna kampuni hiyo inavyotoa elimu ya ufugaji bora wa kisasa kwa wafugaji wanaotembelea maonesho hayo.
Sakulo amesema maonesho ya Nane Nane yana manufaa makubwa kwa wananchi iwapo elimu inayotolewa na wataalamu itawafikia wafugaji na wakulima ili waweze kubadili mbinu za uzalishaji.
Amesema kuwa, Wilaya ya Ngorongoro yenye idadi kubwa ya wafugaji bado inakabiliwa na changamoto ya kufuga kwa njia za jadi, hali inayopunguza tija ya mifugo licha ya kuwa na idadi kubwa ya ng’ombe.
Ameeleza kuwa ,mfugaji anaweza kumiliki maelfu ya ng’ombe lakini asipate faida inayolingana na idadi hiyo, wakati ufugaji wa kisasa wa ng’ombe wachache wenye ubora unaweza kutoa maziwa na nyama nyingi zaidi pamoja na kuongeza kipato cha mfugaji .
Sakulo amewataka wataalamu wa mifugo na taasisi mbalimbali zinazoshiriki maonesho hayo kuendelea kutoa elimu kwa wananchi kuhusu matumizi ya mbegu bora za mifugo na teknolojia za kisasa ili wafugaji waweze kuongeza uzalishaji na kipato.
“Naomba nitumie fursa hii kuwahimiza wadau wanaozalisha na kusambaza mbegu bora za mifugo wakiwemo kampuni ya West Kilimanjaro Ranching kuhakikisha huduma hizo zinawafikia wafugaji wa Ngorongoro kwa urahisi, ili waweze kuanza kufuga mifugo yenye tija badala ya kutegemea mifugo mingi isiyo na uzalishaji wa kuridhisha.”amesema Sakulo.
Amesema mabadiliko hayo pia yatasaidia kupunguza changamoto ya uhaba wa malisho ambayo imekuwa kilio kikubwa cha wafugaji wengi wa Ngorongoro, kwani ufugaji wa kisasa unahitaji idadi ndogo ya mifugo yenye uzalishaji mkubwa.
Aidha Sakrumkola amewataka wananchi kutumia fursa ya maonesho ya Nane Nane kujifunza teknolojia mpya za kilimo na ufugaji ili kuongeza tija, kuboresha kipato cha kaya na kuchangia maendeleo ya uchumi wa wilaya na taifa kwa ujumla.
Kwa upande wake Afisa Mahusiano kutoka kampuni hiyo ,Lee Mamasita amesema kuwa ,amesema kuwa ,kampuni hiyo imewekeza katika uzalishaji wa malisho ili kukabiliana na changamoto ya upungufu wa mvua na ukame unaojitokeza katika maeneo mengi ya wafugaji.
Amesema kampuni hiyo imetekeleza ushauri wa Serikali kwa kulima nyasi aina ya Rhodes Grass, ambazo huvunwa na kuhifadhiwa kwa ajili ya kulisha mifugo wakati wa kiangazi, hatua inayosaidia kuhakikisha mifugo inaendelea kupata lishe bora mwaka mzima.
Mamasita ameongeza kuwa , hadi sasa kampuni hiyo imetekeleza zaidi ya miradi mitano ya maendeleo kwa manufaa ya jamii inayowazunguka.
Aidha, amesema kampuni hiyo inaendelea kushirikiana na ranchi za Taifa katika kuendeleza sekta ya mifugo huku akitolea mfano Ranchi ya NARCO Mkata iliyopo Morogoro, ambayo tayari imepokea mbegu za mbuzi aina ya Boer kutoka kampuni hiyo kwa lengo la kuimarisha uzalishaji wa mbegu bora nchini.
“Nawakaribisha wafugaji, wanafunzi, watafiti na wawekezaji kutembelea ranchi ya West Kilimanjaro ili kujifunza kuhusu teknolojia na mbinu za kisasa za ufugaji wa mifugo bora. na tunaiomba Serikali kuendelea kuwaunga mkono wawekezaji katika sekta ya mifugo kwa kuweka mazingira wezeshi yatakayochochea uzalishaji na upatikanaji wa mbegu bora nchini.”amesema Mamasita .
Amefafania zaidi kuwa kampuni hiyo ipo katika hatua za mwisho za kupata idhini ya Serikali ya kuanzisha kituo maalumu cha uzalishaji wa mbegu za madume na majike wa mifugo ambapo kukamilika kwa kituo hicho kitakuwa na mchango mkubwa katika kuharakisha uboreshaji wa mbegu za mifugo nchini na kuongeza tija katika sekta ya mifugo kwa manufaa ya wafugaji na uchumi wa Taifa.
