Na Meleka Kulwa-Fullshangwe Blog, Dodoma

WAZIRI wa Fedha, Mhe. Balozi Khamis Mussa Omar, ameipa mwelekeo mpya Benki ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania (TADB) kwa kuitaka kuongeza msukumo wa uwekezaji kwenye maeneo ya kilimo yanayolenga kukuza uzalishaji na kufikia malengo ya Serikali katika sekta hiyo.

Ameyasema hayo August 2,2026 wakati alipotembelea banda la TADB katika Maonesho ya Nane Nane ya Kitaifa na Kimataifa yanayoendelea katika Viwanja vya Dk. John Samuel Malecela, Nzuguni jijini Dodoma.

Amesema kuwa kilimo ni sekta muhimu katika kufanikisha mipango ya maendeleo ya taifa, hivyo taasisi za kifedha zinapaswa kuweka mikakati itakayowawezesha wakulima, wafugaji na wavuvi kupata fursa zaidi za mitaji na masoko.

Amebainisha kuwa Serikali imeendelea kuimarisha uwezo wa TADB kwa kuongeza mtaji wake kutoka Sh bilioni 60 hadi zaidi ya Sh bilioni 400, hatua inayolenga kuongeza uwezo wa benki hiyo kutoa huduma za kifedha kwa wadau wengi zaidi wa sekta ya kilimo.

Aidha, ameongeza kuwa utekelezaji wa Dira ya Taifa ya 2050 unahitaji mabadiliko makubwa katika sekta za uzalishaji, hususan kilimo ambacho kina mchango mkubwa katika ajira, kuongeza kipato cha wananchi na kukuza uchumi wa nchi.

“Maendeleo ya kilimo, mifugo, uvuvi na sekta nyingine zinazohusiana yataendelea kuwa msingi wa kufikia malengo makubwa ya kiuchumi ambayo Serikali imejiwekea,” amesema Mhe. Balozi Omar.

Aidha ,amewapongeza wajasiriamali wanaoshiriki katika maonesho hayo kwa kuonesha bidhaa zenye ubora, huku akisisitiza umuhimu wa kuendelea kutafuta masoko mapya ili bidhaa za ndani ziweze kushindana katika soko la kimataifa.

Amesema kuwa Wizara ya Kilimo inapaswa kuendelea kushirikiana na wazalishaji hao kwa kuwawezesha kuongeza uzalishaji, kuboresha ubora wa bidhaa na kupata masoko ya uhakika.

“Bidhaa nyingi tunazoziona hapa zina ubora mzuri, kinachohitajika ni kuongeza juhudi katika kuzitangaza na kuwaunganisha wazalishaji na masoko,” amesema Mhe. Balozi Omar