Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan akiwa kwenye picha na mgeni wake Rais wa Jamhuri ya Kiarabu ya Misri, Mhe. Abdel Fattah El-Sisi, Ikulu Jijini Dar es Salaam, tarehe 18 Julai Juni, 2026.

Rais wa Jamhuri ya Kiarabu ya Misri, Mhe. Abdel Fattah El-Sisi akisaini Kitabu cha Wageni baada ya kuwasili kwenye ukumbi wa Kikwete, Ikulu Jijini Dar es Salaam, tarehe 18 Julai Juni, 2026.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan akiwa kwenye mazungumzo na mgeni wake Rais wa Jamhuri ya Kiarabu ya Misri, Mhe. Abdel Fattah El-Sisi, Ikulu Jijini Dar es Salaam, tarehe 18 Julai Juni, 2026.

…………. 

Na Mwandishi Wetu

DAR ES SALAAM, Julai 18, 2026 – Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, amesema ziara ya kitaifa ya Rais wa Jamhuri ya Kiarabu ya Misri, Mhe. Abdel Fattah El-Sisi, itafungua ukurasa mpya wa kuimarisha ushirikiano wa kiuchumi kati ya mataifa hayo mawili, hususan katika biashara, uwekezaji, kilimo, miundombinu, afya, elimu na sayansi.

Akizungumza na waandishi wa habari Ikulu jijini Dar es Salaam baada ya mazungumzo rasmi na mgeni wake Julai 18, 2026, Dkt. Samia amesema ujio wa Rais El-Sisi, aliyeambatana na ujumbe wa wafanyabiashara na wawekezaji, unatoa fursa ya kujadili kwa kina namna bora za kuimarisha uhusiano wa kihistoria uliodumu kwa miaka mingi kati ya Tanzania na Misri.

Dkt. Samia alibainisha kuwa hiyo si mara ya kwanza kwa Rais El-Sisi kutembelea Tanzania, akieleza kuwa aliwahi kufanya ziara nchini mwaka 2017, jambo linalodhihirisha uimara wa uhusiano wa kidiplomasia na kirafiki kati ya mataifa hayo mawili. Aliongeza kuwa yeye pia alifanya ziara nchini Misri mwaka 2021 na wamekubaliana kufanya ziara nyingine kwa wakati muafaka ili kuendeleza ushirikiano huo.

Alisema urafiki kati ya Tanzania na Misri ulianza hata kabla ya ukoloni kupitia wafanyabiashara wa Misri waliokuwa wakifika katika mwambao wa Afrika Mashariki. Aidha, wakati wa harakati za ukombozi wa Afrika, nchi hizo zilishirikiana kwa karibu na baada ya uhuru ziliendelea kuimarisha ushirikiano katika sekta mbalimbali kupitia Tume ya Pamoja ya Ushirikiano (JCC) iliyoanzishwa mwaka 1989.

Rais Samia aliishukuru Serikali ya Misri kwa mchango wake katika maendeleo ya Tanzania kupitia ufadhili wa mafunzo na masomo kwa Watanzania, pamoja na ushirikiano wa wataalamu wa afya wa nchi hiyo ambao kwa kushirikiana na wataalamu wa Tanzania wamefanikisha upasuaji wa wagonjwa wa moyo zaidi ya 420 katika kipindi cha miaka 10 iliyopita.

Alisema moja ya vielelezo vikubwa vya ushirikiano huo ni utekelezaji wa Mradi wa Kufua Umeme wa Julius Nyerere wenye thamani ya Sh trilioni 7.4, uliojengwa na kampuni mbili kutoka Misri kwa kutumia fedha za ndani za Tanzania.

“Mradi huu ni uthibitisho kwamba nchi za Afrika zikiamua zinaweza kutekeleza miradi mikubwa ya kimkakati kwa uwezo wao wenyewe na bila kutegemea ushiriki wa nje ya bara la Afrika,” amesema.

Kuhusu biashara na uwekezaji, Dkt. Samia amesema pande zote zimekubaliana kuwa kiwango cha biashara kati ya Tanzania na Misri bado ni kidogo licha ya kuwepo kwa fursa kubwa za kukiongeza.

Alisema Misri ni ya nane kati ya nchi 10 zinazoongoza kwa uwekezaji nchini Tanzania, ikiwa na miradi 61 yenye thamani ya dola za Marekani bilioni 1.5 iliyozalisha ajira zaidi ya 4,000 katika sekta za nishati, viwanda, ujenzi, kilimo, utalii na huduma nyingine.

Aidha, amesema wafanyabiashara 35 kutoka Misri wameambatana na Rais El-Sisi na wanakutana na wenzao wa Tanzania kupitia jukwaa la biashara, hatua inayotarajiwa kuongeza biashara na uwekezaji kwa kutumia fursa za Eneo Huru la Biashara la Afrika (AfCFTA).

Katika sekta ya kilimo, Rais Samia amesema Afrika hutumia kati ya dola za Marekani milioni 70 hadi milioni 100 kila mwaka kuagiza chakula kutoka nje, hususan ngano, mahindi, mchele, mafuta ya kula, sukari, nyama na maziwa. Alisema hali hiyo inaonyesha umuhimu wa kuwekeza zaidi katika uzalishaji wa chakula ndani ya bara.

Amesema Tanzania ina hekta milioni 29 zinazofaa kwa kilimo cha umwagiliaji na ni nchi ya pili barani Afrika kwa idadi ya mifugo, huku Misri ikiwa imepiga hatua kubwa katika teknolojia za umwagiliaji kutokana na matumizi ya Mto Nile.

Kwa msingi huo, amesema nchi hizo zimekubaliana kushirikiana katika teknolojia za umwagiliaji na kuendeleza kilimo pamoja na ufugaji, ikiwemo kuwekeza katika Ranchi ya Ruvu pamoja na maeneo yanayomilikiwa na JKT, Magereza, NARCO na Zanzibar.

Katika sekta ya miundombinu, amesema viongozi hao wamekubaliana kuimarisha ushirikiano katika usafiri wa anga, reli na bahari. Misri itashiriki katika maendeleo ya Bandari ya Bagamoyo na kuunganisha bandari hiyo na reli ya kisasa kuelekea Kwala, ambako kutatengwa eneo maalumu la kuhifadhi bidhaa na makontena ya wafanyabiashara wa Misri.

Aidha, amesema EgyptAir itaendelea kufanya safari tatu kwa wiki kati ya Misri na Tanzania, huku Shirika la Ndege Tanzania (ATCL) likijiandaa kuanzisha safari zake kuelekea nchini humo. Pia mazungumzo yanaendelea kuhusu kuanzisha ushirikiano wa usafiri wa baharini utakaounganisha Bandari za Dar es Salaam, Bagamoyo na Sofaga ili kurahisisha biashara kati ya nchi hizo na masoko ya Kusini mwa Afrika.

Katika afya na elimu, Dkt. Samia amesema Misri imeonyesha utayari wa kujenga hospitali mpya yenye vifaa vya kisasa nchini Tanzania pamoja na kuendelea kushirikiana katika mafunzo ya wataalamu wa afya na tiba za magonjwa ya moyo, figo na saratani.

Ameongeza kuwa ameomba Misri ishirikiane na Tanzania katika kuendeleza sayansi na teknolojia kwa kutoa nafasi zaidi za masomo katika maeneo ya akili bandia (AI), usalama wa mtandao, TEHAMA na fani nyingine za kisasa kupitia programu ya Samia Extended Scholarship, ombi ambalo Rais El-Sisi amelkubali.

Aidha, amesema nchi hizo zimekubaliana kuendelea kushirikiana katika usimamizi wa rasilimali za maji, hususan kuhakikisha matumizi ya maji ya Ziwa Victoria yanaendelea kufanyika kwa njia endelevu bila kuathiri mtiririko wa maji kuelekea Mto Nile.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan akiongoza Ujumbe wa Tanzania kwenye mazungumzo rasmi na Ujumbe wa Jamhuri ya Kiarabu ya Misri, uliongozwa na Rais wa nchi hiyo, Mhe. Abdel Fattah El-Sisi, Ikulu Jijini Dar es Salaam, tarehe 18 Julai Juni, 2026.