Mwenyekiti wa Chama cha ACT Wazalendo Taifa, Othman Masoud Othman, amesema kuna watu wamejipanga kuhakikisha makubaliano yaliyofikiwa kati ya chama chake na Chama Cha Mapinduzi (CCM) kwa ajili ya kuondoa mkwamo wa kisiasa Zanzibar hayafanikiwi.

Othman alitoa kauli hiyo Julai 15, 2026, katika Wilaya ya Mkoani, Mkoa wa Kusini Pemba, alipokuwa akizungumza na viongozi na wanachama wa ACT Wazalendo kuhusu hatua zilizofikiwa katika mazungumzo hayo.

Alisema watu hao wanafahamika na wanatumia hoja ya kulinda Mapinduzi ya Zanzibar kama kisingizio cha kupinga utekelezaji wa makubaliano hayo.

«”Hawa ni wa kupambana nao kwa njia zozote ili wasifanikiwe kuturudisha nyuma,” alisema.»

Aliongeza kuwa iwapo kuna watu wasiokubaliana na suluhu hiyo, wanapaswa kujitokeza hadharani na kueleza msimamo wao badala ya kuhujumu mchakato huo kwa njia zisizo wazi.

Othman, ambaye pia ni Makamu wa Kwanza wa Rais wa zamani wa Zanzibar, alitumia rejea za aya za Qur’ani kueleza kuwa tabia ya unafiki imekuwepo tangu enzi za Mitume.

“Licha ya kuingia katika makubaliano haya, chama chetu kitaendelea kuwa imara katika kufuatilia utekelezaji wake na kuzungumza pale panapohitajika,” alisema.

Aliwataka viongozi wa ACT Wazalendo kushirikiana na wenzao wa CCM kuhakikisha makubaliano yote yanatekelezwa kwa uaminifu, akisisitiza kuwa huu ni wakati wa kujenga imani na kuachana na majungu pamoja na mivutano ya kisiasa.

“Nawaomba sana viongozi wenzangu wa Chama Cha Mapinduzi kuyatekeleza kwa dhati yale tuliyokubaliana kwa maslahi ya nchi yetu na vizazi vijavyo,” alisema.

Othman alisisitiza kuwa lengo la mazungumzo hayo halikuwa kuwanufaisha CCM wala ACT Wazalendo, bali kuhakikisha Wazanzibari wanapata mazingira bora ya amani, maendeleo na ustawi wa kudumu.

Alisema makubaliano hayo yakitekelezwa kwa uaminifu, Zanzibar inaweza kupiga hatua kubwa kiuchumi na kuwa mfano wa kuigwa katika ukanda wa Afrika Mashariki.

Akizungumzia taarifa zinazotolewa kwa wanachama, alisema viongozi hawaelezi siri za vikao bali matokeo ya maamuzi yaliyofikiwa kwa pamoja.

Kwa upande wake, Makamu Mwenyekiti wa ACT Wazalendo Zanzibar, Ismail Jussa, alisema Watanzania wengi wana matumaini makubwa na chama hicho katika kuendeleza ajenda ya mabadiliko ya kisiasa nchini.

“Viongozi, nawaombeni tusiwachanganye wafuasi wetu, kwani chama chetu kimebeba matumaini makubwa ya Watanzania,” alisema Jussa.

Naye Makamu Mwenyekiti wa ACT Wazalendo Tanzania Bara, Is-Haka Rashid Mchinjita, aliwataka wanachama wa chama hicho Pemba kuendelea kuimarisha mshikamano ili kufanikisha malengo ya kisiasa waliyojiwekea.

Ziara ya siku mbili ya viongozi wa juu wa ACT Wazalendo ya kueleza wanachama yaliyofikiwa katika makubaliano ya kuondoa mkwamo wa kisiasa Zanzibar ilihitimishwa Julai 15, 2026, baada ya mikutano iliyofanyika katika wilaya za Mkoani na Chake Chake.