Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mhe. Dkt. Hussein Ali Mwinyi, amesema Serikali inaendelea kutekeleza mikakati mbalimbali ya kumaliza tatizo la upatikanaji wa maji katika mikoa yote ya Zanzibar, ili kuhakikisha wananchi wanapata huduma ya maji safi na salama kwa uhakika.
Rais Dkt. Mwinyi ameyasema hayo leo, tarehe 15 Julai 2026, alipokutana na Waziri wa Maji, Nishati na Madini Zanzibar, Mhe. Nadir Abdullatif, pamoja na ujumbe wa Wizara ya Maji ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, ulioongozwa na Waziri wa Maji, Mhe. Jumaa Aweso, waliofika Ikulu Zanzibar kwa mazungumzo.
Amesema baadhi ya mikoa tayari imenufaika na uwekezaji pamoja na ujenzi wa miradi mikubwa ya maji, inayolenga kuondoa changamoto zinazowakabili wananchi katika kupata maji safi na salama. Ameitaja mikoa hiyo kuwa ni Kaskazini Unguja, Kusini Unguja na Mjini Magharibi.
Rais Dkt. Mwinyi amesema sekta ya maji ni muhimu kwa maendeleo na ustawi wa jamii, ambapo miradi mbalimbali inaendelea kutekelezwa katika maeneo mengi ya Zanzibar, kwa lengo la kuhakikisha huduma hiyo inapatikana kwa urahisi, uhakika na wakati wote.
Aidha, ameishauri Wizara ya Maji, Nishati na Madini Zanzibar kuendelea kujifunza kutoka Wizara ya Maji ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kuhusu usimamizi na utekelezaji wenye ufanisi wa miradi ya maji.
Amesisitiza umuhimu wa matumizi ya teknolojia za kisasa katika sekta hiyo na kuitaka wizara kwenda sambamba na mabadiliko ya kiteknolojia, ili kuimarisha utekelezaji, usimamizi endelevu wa miradi ya maji.
Rais Dkt. Mwinyi ameipongeza Wizara ya Maji, Nishati na Madini Zanzibar kwa kuandaa mipango ya utekelezaji wa miradi mikubwa ya maji, ambayo itasaidia kumaliza tatizo la upatikanaji wa maji safi na salama katika mikoa yote ya Zanzibar.
Naye Waziri wa Maji wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Jumaa Aweso, amempongeza Rais Dkt. Mwinyi kwa utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo inayosimamiwa na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar.
Ameahidi kuwa wizara yake itaendelea kutoa ushirikiano unaohitajika ili kufanikisha utekelezaji wa miradi hiyo yenye umuhimu mkubwa kwa ustawi wa wananchi wa Zanzibar.
Aidha, amesema Wizara ya Maji tayari imeandaa mfumo maalumu unaotumia teknolojia, utakaowawezesha wananchi kutoa taarifa kuhusu changamoto za huduma ya maji na kusaidia mamlaka husika kuzitatua kwa haraka na ufanisi.

