Na Silivia Amandius 

Kagera.

Naibu Waziri wa Madini, Dkt. Steven Kiruswa, amesema Serikali haitavumilia vitendo vya utoroshaji wa madini na kwamba hatua kali za kisheria zitaendelea kuchukuliwa dhidi ya wote wanaojihusisha na biashara hiyo haramu.

Akizungumza mkoani Kagera Leo July 13, mwaka huu Dkt. Kiruswa amesema Serikali imefanikiwa kukamata watuhumiwa kadhaa waliokuwa wakijaribu kutorosha madini ya dhahabu na vito kupitia operesheni mbalimbali zilizofanywa kwa ushirikiano wa vyombo vya dola.

Katika operesheni ya tarehe 29 Juni 2026 iliyofanyika eneo la Benako, wilayani Ngara, polisi walikamata gari lililokuwa limebeba viroba 20 vya madini ya vito. Uchunguzi ulionyesha madini hayo yalikuwa na uzito wa kilo 627.229, yenye thamani ya zaidi ya shilingi milioni 10.9, huku kodi ya Serikali ikiwa zaidi ya shilingi milioni 1.01. Mmiliki wa madini hayo alikiri kosa la kukwepa kulipa makosa na faini kwa mujibu wa Sheria ya Madini.

Aidha, tarehe 1 Julai 2026, askari walimkamata mtuhumiwa mwingine akiwa ndani ya gari la International Transit (IT) akimiliki dhahabu yenye uzito wa gramu 4,434.66, yenye thamani ya zaidi ya shilingi bilioni 1.34, huku kodi ya Serikali iliyokuwa ikipaswa kulipwa ikiwa zaidi ya shilingi milioni 125.8.

Vilevile, tarehe 4 Julai 2026, mshirika wa mtuhumiwa huyo alikamatwa akiwa na dhahabu yenye uzito wa gramu 453, yenye thamani ya zaidi ya shilingi milioni 144.2. Mtuhumiwa huyo ameunganishwa kwenye kesi inayoendelea mahakamani.

Akihitimisha taarifa hiyo, Naibu Waziri wa Madini, Dkt. Steven Kiruswa, amewataka wachimbaji na wafanyabiashara wa madini kuzingatia sheria, kanuni na taratibu za sekta ya madini ili kuepuka migogoro na hatua za kisheria. Pia ametoa wito kwa wananchi kuendelea kushirikiana na vyombo vya dola kwa kutoa taarifa za vitendo vya utoroshaji wa madini na uhalifu mwingine, ili kulinda rasilimali za taifa na kuongeza mapato ya Serikali.