Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe. Dkt. Hussein Ali Mwinyi akiwa kwenye picha na Mwenyekiti wa Chama cha ACT-Wazalendo Taifa Mhe. Othman Masoud Othman baada ya kushuhudia utiaji saini wa ajenda zilizokubaliwa na pande zote mbili kwa ajili ya kufanyiwa kazi kufuatia Tamko la Pamoja la Muafaka wa Kisiasa baina ya Chama cha Mapinduzi (CCM) na ACT-Wazalendo, katika viwanja vya Ikulu Zanzibar tarehe 09 Julai, 2026.
………….
Na Mwandishi Wetu, Zanzibar
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt. Hussein Ali Mwinyi, amesema kutiwa saini kwa tamko la pamoja la maridhiano kati ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) na ACT Wazalendo ni hatua muhimu ya kihistoria itakayofungua ukurasa mpya wa umoja wa kitaifa, utulivu wa kisiasa na maendeleo endelevu kwa Zanzibar.
Dkt. Mwinyi aliyasema hayo leo Julai 9, 2026, Ikulu Zanzibar wakati wa hafla ya utiaji saini wa maridhiano kati ya CCM na ACT Wazalendo, iliyohudhuriwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Mwenyekiti wa CCM, Dkt. Samia Suluhu Hassan, viongozi wa vyama vya siasa, viongozi wa dini, mabalozi wa nchi mbalimbali pamoja na viongozi wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Alisema tamko hilo la pamoja ni hatua muhimu katika jitihada za kufanikisha maridhiano ya kisiasa na kuimarisha mshikamano wa wananchi wa Zanzibar, hali ambayo itasaidia kuharakisha maendeleo ya kiuchumi na kijamii kwa manufaa ya wananchi wote.
“Hatua hii ya leo ni muhimu sana kwa wananchi wa Zanzibar na Watanzania kwa ujumla katika kuimarisha mshikamano, maridhiano ya kitaifa na kufanikisha jitihada zetu za maendeleo,” alisema Dkt. Mwinyi.
Rais huyo aliwashukuru wajumbe wa kamati iliyosimamia awamu ya kwanza ya mazungumzo kwa kazi kubwa waliyoifanya kwa kuweka mbele maslahi ya Zanzibar badala ya maslahi binafsi au ya kisiasa. Pia alitoa shukrani maalumu kwa Marais Wastaafu wa Zanzibar, Dkt. Amani Abeid Karume na Dkt. Ali Mohamed Shein, pamoja na viongozi wa ACT Wazalendo akiwemo Mwenyekiti wa chama hicho, Othman Masoud Othman, na Makamu Mwenyekiti Juma Duni Haji, kwa mchango wao katika kufanikisha hatua hiyo.
Alieleza kuwa maridhiano hayo yanafungua njia ya utekelezaji wa matakwa ya Katiba ya Zanzibar ya mwaka 1984 kuhusu kuendeleza umoja wa kitaifa, huku akiahidi kushirikiana na viongozi wa pande zote kusimamia awamu ya pili ya mchakato huo kwa uadilifu na uwazi.
Kwa mujibu wa Dkt. Mwinyi, hatua inayofuata itahusisha mazungumzo ya kina kuhusu ajenda zilizokubaliwa, kwa kuhakikisha maslahi ya Zanzibar yanawekwa mbele ili kujenga mustakabali bora wa nchi hiyo.
Aidha, alisema mafanikio ya maridhiano hayo yataongeza imani kwa wananchi, wawekezaji, wafanyabiashara na washirika wa maendeleo, jambo litakalosaidia kuvutia uwekezaji zaidi na kuchochea ukuaji wa uchumi wa Zanzibar.
“Ninaamini mwafaka tunaoukusudia utaongeza imani kwa wananchi na wadau mbalimbali, wakiwemo wawekezaji na washirika wa maendeleo, katika kuendelea kushirikiana na Zanzibar kutekeleza mipango yetu ya maendeleo,” alisema.
Dkt. Mwinyi alibainisha kuwa Zanzibar ina historia ya mafanikio katika maridhiano ya kisiasa, akirejea mchakato uliosababisha kufanyika kwa marekebisho ya Katiba na kuundwa kwa Serikali ya Umoja wa Kitaifa, akisema uzoefu huo unatoa matumaini kuwa safari ya sasa pia itafanikiwa.
Aliwataka viongozi wa vyama vya siasa, viongozi wa dini, asasi za kiraia na wananchi wote kuunga mkono mchakato huo kwa dhati, akisisitiza kuwa maendeleo ya Zanzibar yanategemea mshikamano, amani na ushirikiano wa wananchi wake.
Akihitimisha hotuba yake, Dkt. Mwinyi alimshukuru Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, viongozi wa CCM katika ngazi mbalimbali, wajumbe wa kamati zilizoshiriki mazungumzo, wageni waalikwa na vyombo vya habari kwa mchango wao katika kufanikisha hafla hiyo, huku akiwaombea wananchi waendelee kudumisha amani na umoja ili Zanzibar izidi kupiga hatua za maendeleo.

