Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam

Mtendaji Mkuu wa Watumishi Housing Investment (WHI), Mhandisi Sephania Solomon, amesema Mfuko wa Uwekezaji wa Faida Fund umeendelea kufanya vizuri baada ya kukusanya zaidi ya shilingi bilioni 100 tangu ulipoanzishwa mwaka 2022 kwa mtaji wa awali wa shilingi bilioni 12, huku ukiendelea kutoa gawio shindani la zaidi ya asilimia 13 kwa wawekezaji.

Akizungumza Julai 9, 2026 alipotembelea banda la WHI na mabanda mengine katika Maonesho ya 49 ya Kimataifa ya Biashara ya Dar es Salaam (Sabasaba), Arch. Solomon alisema mafanikio hayo yanaonesha imani kubwa ya Watanzania katika mfuko huo na kuwataka wananchi wa kada zote kutumia fursa hiyo kujenga uhuru wa kifedha.

“Mpaka tunafunga mwaka, Faida Fund imekusanya zaidi ya shilingi bilioni 100 kutoka bilioni 12 tulizoanza nazo mwaka 2022. Tunaendelea kutoa gawio la zaidi ya asilimia 13, hivyo tunawaalika Watanzania wote kuwekeza kupitia mfumo wetu wa kidijitali ambao ni rahisi na salama,” alisema.

Alieleza kuwa mwekezaji anaweza kuanza kuwekeza akiwa popote bila kufika ofisini, huku mfumo wa kidijitali ukimwezesha kuona uwekezaji wake ukianza kufanya kazi mara moja baada ya kukamilisha hatua za uwekezaji.

Mbali na huduma za uwekezaji, Arch. Solomon aliwataka watumishi wa umma, wanachama wa mifuko ya hifadhi ya jamii na Watanzania wote kutembelea banda la WHI ili kupata taarifa kuhusu miradi ya nyumba za gharama nafuu inayotekelezwa na taasisi hiyo.

Alisema katika mradi unaoendelea jijini Dodoma, nyumba 66 zinatarajiwa kukamilika mwezi Februari 2027, huku nyumba zaidi ya 120 zikitarajiwa kukamilika katika hatua inayofuata ya utekelezaji. Aliongeza kuwa wanunuzi wanaweza kujaza fomu, kupata namba ya malipo na kuanza kulipia nyumba hata wakati ujenzi ukiendelea.

Aidha, alisema WHI inajiandaa kuanza mradi mkubwa wa zaidi ya nyumba 250 katika eneo la Mbezi Beach, Jangwani jijini Dar es Salaam, huku miradi mingine ikiendelea kupanuliwa katika maeneo mbalimbali nchini.

“Tumejenga zaidi ya nyumba 132 kwa watumishi wa umma na mwaka huu tunatarajia kujenga nyingine zaidi ya 132, hivyo kufikisha zaidi ya nyumba 264. Lengo letu ni kuhakikisha watumishi wa umma wanapata makazi bora na ya gharama nafuu ili waendelee kufanya kazi kwa tija,” alisema.

Alibainisha kuwa WHI itaendelea kutekeleza miradi ya nyumba katika mikoa mbalimbali ikiwemo Kigoma, Serengeti pamoja na maeneo ya visiwani kama Ukerewe na Mafia, kwa lengo la kuwafikia watumishi wa umma na wananchi wengi zaidi.

Mhandisi Solomon alisisitiza kuwa banda la WHI katika Maonesho ya Sabasaba linatoa elimu kuhusu uwekezaji, umiliki wa nyumba na huduma nyingine zinazotolewa na taasisi hiyo, huku akiwakaribisha Watanzania wote kufika kupata maelezo na kunufaika na fursa zilizopo.