Waziri wa Nchi ofisi ya waziri mkuu Tamisemi Prof Riziki Shemdoe wakati akizungumza katika uzinduzi wa mafunzo ya uwezeshaji wananchi kiuchumi yaliyofanyika Sumbawanga Mkoani Rukwa.

Baadhi ya washiriki makundi maalumu wakiwa katika picha ya pamoja na waziri wa Nchi ofisi ya waziri mkuu Tamisemi Prof Riziki Shemdoe
…………
Na Neema Mtuka, Sumbawanga
RUKWA: Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (TAMISEMI), Prof. Riziki Shemdoe, amesema dhamira ya Serikali ni kuhakikisha inaboresha huduma kwa wananchi na kutatua changamoto kwa wakati ili miradi ya maendeleo itekelezwe kwa ufanisi mkubwa.
Prof. Shemdoe amesema hayo leo Julai 13, 2026, katika uzinduzi wa mafunzo ya utoaji wa elimu kuhusu fursa za mitaji kupitia mifuko ya kuwawezesha wananchi kiuchumi, yaliyofanyika Sumbawanga mkoani Rukwa.
Akizungumza katika mafunzo hayo, Prof. Shemdoe amewahimiza wakurugenzi kote nchini kusajili vikundi mbalimbali na kuwapa mikataba ya kusafisha barabara na mitaro.
“Niwaombe wakurugenzi wote kusimamia na kuratibu mikopo ya asilimia 10 ili wananchi wote wanufaike na mikopo hiyo bila upendeleo,” amesema Prof. Shemdoe.
Awali, akimkaribisha mgeni rasmi, Mkuu wa Mkoa wa Rukwa, Charles Makongoro Nyerere, amesema mkoa huo umetekeleza miradi mikubwa ya maendeleo, ikiwemo ujenzi wa Uwanja wa Ndege wa Sumbawanga wenye thamani ya shilingi bilioni 60.1.
Makongoro amewasisitiza washiriki wa mafunzo hayo kuyafanyia kazi yote watakayofundishwa ili wanufaike na uwezeshaji huo.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Halmashauri ya Manispaa ya Sumbawanga, Pendo Mangali, amesema halmashauri imepiga hatua kubwa katika kuleta maendeleo kwa wananchi, ikiwemo utoaji wa mikopo inayowapa fursa ya kuongeza mitaji kwenye biashara zao.
“Mikopo hii ni endelevu na tutaendelea kuitoa kulingana na ukusanyaji wa mapato yetu,” amesisitiza Mangali.
Baadhi ya wananchi walioshiriki katika mafunzo hayo, akiwemo Raymond Makelele, mkazi wa Sumbawanga, wameitaka Serikali kuendelea kuwawezesha wananchi kiuchumi, wakisema elimu waliyoipata itawasaidia kujiinua kiuchumi.
“Serikali iendelee kuwawezesha wananchi kiuchumi, jambo ambalo litawajengea uwezo wa kutoka katika hali duni ya maisha,” amesema Makelele.
Mratibu wa mafunzo ya uwezeshaji wananchi kiuchumi, ambaye pia ni Mbunge wa Viti Maalumu Mkoa wa Rukwa, Jacqueline Mzindakaya, amesema lengo la mafunzo hayo ni kuwainua wananchi kiuchumi na kuwakumbusha fursa zilizopo pamoja na namna ya kuzichangamkia ili kukuza kipato cha mtu mmoja mmoja na taifa kwa ujumla.
Mafunzo hayo yamewakutanisha wananchi, wajasiriamali, vikundi vya wanawake na vijana, makundi yenye mahitaji maalumu, pamoja na wadau mbalimbali wa maendeleo.
