CHENNAI, INDIA, Julai 18, 2026 – Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt. Hussein Ali Mwinyi, amewatembelea wagonjwa kutoka Zanzibar wanaopatiwa matibabu katika Hospitali ya MIOT International jijini Chennai, India, kupitia udhamini wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar.

Katika ziara hiyo, Rais Dkt. Mwinyi aliwajulia hali wagonjwa hao, akazungumza nao pamoja na familia zao na kupokea taarifa kutoka kwa madaktari kuhusu maendeleo ya matibabu wanayopatiwa.

Sambamba na ziara hiyo, Rais Dkt. Mwinyi alikutana na madaktari bingwa wa Zanzibar wanaopata mafunzo kupitia Samia Health Super-Specialization Scholarship Program, na kusisitiza umuhimu wa kutumia maarifa na utaalamu wanaoupata ili kuimarisha huduma za afya nchini.

Alisema Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar itaendelea kuwekeza katika sekta ya afya kwa kuimarisha huduma za kibingwa, kuongeza mafunzo kwa wataalamu wa afya na kupanua ushirikiano na taasisi za kimataifa ili wananchi wapate huduma bora zaidi.

Rais Dkt. Mwinyi alieleza kuwa uwekezaji huo unalenga pia kupunguza idadi ya wagonjwa wanaolazimika kwenda nje ya nchi kutafuta matibabu, kwa kujenga uwezo wa wataalamu na kuboresha huduma za kibingwa ndani ya Zanzibar na Tanzania kwa ujumla.