NA DENIS MLOWE, IRINGA
WADAU wa soka mkoani Iringa wameanza kuweka mikakati ya pamoja ya kuhakikisha mkoa unapata tena timu ya Ligi Kuu Tanzania Bara, huku wakisisitiza kuwa mafanikio hayo yatawezekana endapo yatajengwa juu ya misingi imara ya uongozi, miundombinu, uwazi na ushirikiano wa wadau wote.
Katika kikao kilichowakutanisha viongozi wa soka, makocha, wadau wa michezo na viongozi wa taasisi mbalimbali, washiriki walikubaliana kuwa kurejesha hadhi ya soka la Iringa kunahitaji maandalizi ya kina badala ya hatua za haraka zisizo na msingi wa kudumu.
Akizungumza katika kikao hicho, Kiongozi wa Chama cha Soka Mkoa wa Iringa (IRFA), Cyprian Kuyava, alisema ndoto ya kuwa na timu ya Ligi Kuu haiwezi kutimia kwa hisia pekee bali inahitaji uwekezaji wa muda mrefu, mfumo madhubuti wa uendeshaji pamoja na taasisi au wadhamini wenye uwezo wa kuiendesha timu kwa ufanisi.
Alisema timu haiwezi kutegemea michango ya hapa na pale kwa sababu gharama za usafiri, maandalizi, mishahara na uendeshaji wa msimu mzima ni kubwa, hivyo ni lazima kuwe na mfumo endelevu wa kifedha na uongozi wa kitaalamu.
Kwa mujibu wake, hata kama timu itashuka daraja, hilo lisigeuke chanzo cha lawama bali liwe sehemu ya kujifunza na kuboresha mifumo ya uendeshaji ili kuhakikisha maendeleo ya muda mrefu.
Kwa upande wake, Dk. Kenny Ally alisema kabla ya kufikiria namna ya kupata timu, jambo la kwanza ni kuhakikisha Iringa inakuwa na uwanja wenye viwango vinavyokubalika kwa mashindano ya Ligi Kuu.
Alisema historia imeonyesha kuwa timu zinazokosa viwanja vya nyumbani hulazimika kuhamahama kucheza katika mikoa mingine, hali inayozipunguzia ushindani na kuwanyima mashabiki fursa ya kuziunga mkono.
“Uwanja ndiyo msingi wa kila kitu. Tukijenga mazingira bora ya uwanja, hata kuvutia wawekezaji na timu itakuwa rahisi zaidi,” alisema.
Kocha wa timu za vijana mkoani Iringa, Said Chitalula, alisema umiliki wa timu unapaswa kubaki mikononi mwa taasisi au wawekezaji wenye uwezo wa kifedha, huku jukumu la wadau likiwa ni kutoa ushirikiano, hamasa na kuhakikisha mazingira yanakuwa rafiki kwa maendeleo ya timu.
Alisema Iringa inapaswa kujifunza kutokana na sababu zilizosababisha kupoteza timu zake za zamani ili makosa hayo yasijirudie, akisisitiza kuwa mshikamano wa wananchi na wadau ndio utakaowezesha timu yoyote itakayokuja kupata mafanikio.
Chitalula aliongeza kuwa pamoja na umuhimu wa kuwapa nafasi vijana wa Iringa, timu ya ushindani inahitaji pia kusajili wachezaji bora kutoka maeneo mbalimbali nchini ili kuongeza ubora wa kikosi.
Mwenyekiti wa Chama cha Waamuzi Mkoa wa Iringa na Makamu Mwenyekiti wa Chama cha Waamuzi Tanzania, Kasanga Michael, alisema ni makosa kuendelea kulaumu IRFA kila timu inaposhuka daraja kwa kuwa jukumu la chama hicho ni kusimamia sheria, kanuni na taratibu za mchezo, si kuendesha timu.
Alisema kikao hicho kimetoa nafasi ya wadau kuelewa majukumu ya kila taasisi na kubainisha maeneo yanayohitaji kuboreshwa, ikiwemo mawasiliano, usimamizi wa soka na ujenzi wa ushirikiano baina ya wadau.
Kasanga alisisitiza kuwa pamoja na masuala ya masoko na kutafuta wadhamini, uadilifu wa viongozi watakaopewa dhamana ya kusimamia timu ndio utakaokuwa msingi wa mafanikio ya muda mrefu
Naye David Wapalila alipendekeza njia mbili za kuifikisha Iringa Ligi Kuu, ambazo ni kununua timu iliyopo Championship au First League na kuipandisha, au kuanza na timu ya mkoa na kuijenga hatua kwa hatua hadi kufikia Ligi Kuu.
Alisema kununua timu ya Ligi Kuu moja kwa moja ni jambo gumu kutokana na gharama kubwa, hivyo ni busara kuangalia timu za madaraja ya chini ambazo zinaweza kupandishwa kwa mpango maalumu.
Aidha, alisisitiza kuwa kabla ya kufanya ua
Kununua timu ni lazima kuwepo bajeti ya kuiendesha kwa msimu mzima pamoja na mkakati wa muda mrefu wa maendeleo ya klabu.
Kwa upande wake, Abuu Changawa Majeki alisema jambo muhimu ni kuhakikisha wananchi wa Iringa wanaendelea kuungamkono juhudi zozote zitakazofanywa na wadau wa kurejesha timu ya Ligi Kuu.
Alisema bila kujali timu itamilikiwa na nani, jambo la msingi ni kuweka mikakati ya pamoja, kuondoa migawanyiko na kuhakikisha kila mdau anatoa mchango wake ili ndoto ya Iringa kuwa na timu ya Ligi Kuu itimie.
Kwa ujumla, kikao hicho kimeweka msingi wa mwanzo wa safari ya kurejesha soka la ushindani mkoani Iringa, huku wadau wakikubaliana kuwa mafanikio yatategemea uwepo wa uongozi wenye uwazi, miundombinu bora, uwekezaji wa kutosha na mshikamano wa wananchi wote.

