Timu ya Taifa ya Canada imekuwa timu ya kwanza kutinga hatua ya 16 Bora ya Kombe la Dunia 2026 baada ya kuibuka na ushindi wa mabao 1-0 dhidi ya Afrika Kusini katika mchezo wa hatua ya 32 Bora uliochezwa nchini Marekani.
Baada ya dakika 90 kumalizika kwa sare ya 0-0, Canada ilipata bao la ushindi katika muda wa nyongeza kupitia kwa Stephen Eustรกquio, aliyefunga dakika ya 90+2 kwa shuti kali kufuatia walinzi wa Afrika Kusini kushindwa kuondoa mpira ipasavyo.
Kwa ushindi huo, Canada itakutana na mshindi wa mchezo kati ya Uholanzi na Morocco katika hatua ya 16 Bora.
Canada, ambayo ni mmoja wa waandaaji wenza wa Kombe la Dunia 2026 pamoja na Marekani na Mexico, ilionyesha kiwango bora kwa sehemu kubwa ya mchezo licha ya kumiliki mpira kwa asilimia 42 dhidi ya asilimia 58 za Afrika Kusini.
Katika takwimu za mchezo, Canada ilitengeneza nafasi nne za wazi za kufunga na kupiga mashuti saba yaliyolenga lango, huku Afrika Kusini ikipiga shuti moja pekee lililolenga lango.
Pamoja na mashambulizi ya mara kwa mara kutoka Canada, Afrika Kusini ilionyesha uimara mkubwa katika safu yake ya ulinzi hadi iliporuhusu bao la dakika za mwisho.
Afrika Kusini inaaga mashindano baada ya kufuzu hatua ya mtoano kwa kumaliza nafasi ya pili katika Kundi A ikiwa na pointi nne, nyuma ya Mexico iliyomaliza kileleni mwa kundi hilo kwa pointi tisa.
Korea Kusini ilimaliza nafasi ya tatu kwa pointi tatu, huku Czech ikishika mkia kwa pointi moja.
Canada nayo ilifuzu hatua ya mtoano baada ya kumaliza nafasi ya pili katika Kundi B kwa pointi nne.
