Na Mwandishi wetu, Mirerani 

TIMU za soka za mikoa mitatu ya kanda ya kaskazini ya Manyara, Arusha na Kilimanjaro, za vijana wa chini ya miaka 11, 13 na 15 wameshiriki michuano ya Tanzanite CUP 2026.

Mkurugenzi wa uwanja wa Tanzanite complex Charles Mnyalu amesema michuano hiyo imefanyika kwa muda wa siku mbili mji mdogo wa Mirerani wilayani Simanjiro.

Mnyalu amesema michuano hiyo ya Tanzanite CUP 2026 imefanyika katika makundi matatu tofauti ya wavulana wa umri wa miaka 11, 13 na 15.

Amesema michuano hiyo imewashirikisha wachezaji hao vijana wa soka kutoka katika mikoa ya Manyara, Arusha na Kilimanjaro.

Amesema lengo la michuano hiyo ni kuibua na kuendeleza na kukuza kwa vipaji vya watoto hao tangu wakiwa wadogo.

“Michuano hii ya Tanzanite CUP 2026 imeshindanisha vipaji kwa vijana hao kutoka mikoa mitatu ya kanda ya kaskazini,” amesema Mnyalu.

Amewataja mabingwa wa michuano hiyo ni Tanzanite Sports Academy ya mkoa wa Manyara walioshinda kwa umri wa chini ya miaka 15 na walipata kombe.

Amesema timu ya Kilimanjaro Talent ilifanikiwa kuibuka bingwa wa michuano hiyo kwa upande wa chini ya umri wa miaka 11 na 13.

Ameeleza kwamba mwezi Septemba mwaka 2026 wanatarajia pia kufanya mashindano mengine ya watoto katika kuendelea kuibua vipaji vya soka kwa watoto.

Mmoja kati ya wachezaji walioshiriki michuano hiyo Andrew Lyimo wa timu ya Tanzanite Sports Academy amesema vijana wengi wameonyesha vipaji vyao katika mashindano ya Tanzanite CUP 2026.

Lyimo amempongeza Mnyalu kwa kuandaa michuano hiyo ambayo inawaandaa vijana wadogo kuwa wachezaji mahiri kwa miaka ya baadaye.

“Wadau wa maendeleo wamuunge mkono mkurugenzi wetu Mnyalu ambaye amekuwa mstari wa mbele katika kunyanyua vipaji vya vijana wadogo wanaocheza soka,” amesema Lyimo.