YAS Tanzania imeongeza juhudi za kuwawezesha wafanyabiashara wadogo na wa kati (SMEs), hususan waanzilishi wa biashara mpya (startups), kupitia programu maalum ya kujenga uwezo inayolenga kuwapatia ujuzi, maarifa ya biashara na suluhisho za kidijitali kwa ajili ya kujenga biashara endelevu na zenye ushindani.

Kupitia kitengo chake cha Yas Business, kwa kushirikiana na Chama cha Biashara cha Ufaransa na Tanzania (FTCC), kampuni hiyo ya mawasiliano imeanzisha programu ya miezi sita ya kujengea uwezo inayojulikana kama ‘Masterclass Series’, inayolenga kuwasaidia startups kukabiliana na changamoto za kuanzisha na kukuza biashara zao.

Mkuu wa Kitengo cha SMEs wa Yas Business, Bw. Gabriel Ndobho, amesema mpango huo unalenga startups na wafanyabiashara wadogo kutokana na nafasi yao kubwa katika kuchochea ukuaji wa uchumi na kuongeza fursa za ajira nchini.

Amesema kupitia mpango huo, wajasiriamali wanapatiwa maarifa ya vitendo pamoja na suluhisho za kidijitali zitakazowawezesha kujenga biashara imara na zenye mafanikio.

“Tunawawezesha wajasiriamali hawa kupata maarifa ya vitendo na suluhisho za kidijitali zitakazowasaidia kujenga biashara zenye uimara na mafanikio,” amesema.

Programu hiyo inajikita katika maeneo mbalimbali muhimu ikiwemo usimamizi wa fedha, masoko, mikakati ya biashara, mabadiliko ya kidijitali na matumizi ya teknolojia, hatua ambazo zitasaidia SMEs kuongeza ufanisi, kupanua masoko na kukuza biashara zao kwa muda mrefu.

Aidha, mpango huo ni sehemu ya mkakati wa Yas Business wa kujenga ushirikiano wa muda mrefu na wajasiriamali kwa kuunganisha elimu ya biashara, ubunifu wa kidijitali na msaada wa kifedha ili kuimarisha mazingira ya ukuaji wa SMEs nchini.

Katika programu hiyo iliyohudhuriwa na karibu startups 60, washiriki walijifunza kuhusu Business Model Canvas, mfumo unaowasaidia wajasiriamali kuelewa vipengele muhimu vya biashara zao ikiwemo uendeshaji, vyanzo vya mapato, gharama, wateja na washirika wa kimkakati.

Mkurugenzi wa Nchi wa Road to Success, Bw. Rodrick Nabe, amewataka waanzilishi wa startups kuwa na mtazamo wa ujasiriamali unaolenga kutatua changamoto za jamii badala ya kusubiri kuwa na mtaji mkubwa kabla ya kuanza biashara.

Amesema wajasiriamali wanaweza kuanza na rasilimali chache na kukuza biashara zao hatua kwa hatua endapo watakuwa na maono, nidhamu na uwezo wa kujenga timu bora.

“Moja ya changamoto kubwa inayowakabili waanzilishi wa startups ni kusita kugawa majukumu kwa wengine, jambo ambalo mara nyingi linazuia ukuaji wa biashara,” amesema.

Amehimiza matumizi ya masoko ya kidijitali, mitandao ya kijamii na zana za akili bandia (AI) kama njia rahisi na yenye gharama nafuu ya kutangaza biashara na kuboresha ufanisi wa shughuli mbalimbali.

Kwa upande wake, mwakilishi wa Charge Africa Limited, Bw. Tony Mlela, amepongeza mpango huo akisema ni jukwaa muhimu la kuwapatia startups maarifa na ujuzi wa kujenga biashara endelevu.

Amesema changamoto mojawapo inayozikabili startups ni kujikita zaidi katika gharama na mtiririko wa fedha huku wakisahau maeneo mengine muhimu ya usimamizi wa biashara.

Ameongeza kuwa kupitia programu hiyo, wajasiriamali wataweza kuziba mapungufu hayo na kupata zana zitakazowasaidia kujenga biashara imara na zenye mafanikio.