Waziri wa Ujenzi, Abdallah Ulega, ameagiza kujengwa kwa kasi zaidi kwa miradi ya miundombinu itakayohusika na Mashindano ya AFCON ambayo Tanzania itakuwa mwenyeji mwakani.
Ulega ameyasema hayo leo mjini Arusha wakati akikagua maendeleo ya ujenzi wa barabara ya Mbauda – Losinyai yenye urefu wa km 70 ambayo ni miongoni mwa barabara muhimu kwa AFCON.
“Nimekagua barabara hii na nimemsisitiza Mkandarasi kuongeza idadi ya vifaa, watalaam na wafanyakazi wa kutosha katika mradi huo na kuweka kambi zinazojitegemea ili kuondoa ucheleweshaji wa kuhamisha vifaa na mitambo kutoka eneo moja hadi jingine”, amesisitiza Ulega.
Barabara hiyo inajengwa na mkandarasi, kampuni ya China Civil Engineering Cinstruction Corporation (CCECC) na inahusu barabara ya Mbauda – Losinyai (km 70) hususan sehemu ya barabara Mbauda – Morongo hadi Makutano ya Arusha na T/Packers (Moshono) hadi Kiserian (km 13).
Waziri huyo amemtaka Mkandarasi huyo kufanya kazi kazi usiku na mchana ili mradi huo ukamilike viwango vya ubora kabla ya kuanza kwa AFCON.
Barabara hiyo inajengwa kuwa njia nne kwa utaratibu wa Sanifu, Jenga.
Ulega ameeleza kuwa Mhe Rais Dkt. Samia Suluhh Hassan ameendeela kutoa kipaumbele kwa ujenzi wa miundombinu ya kisasa ili kuboresha maisha ya wananchi na kukuza pato la Taifa.
Ameongeza kuwa mradi huo ni sehemu ya mkakati wa Serikali wa kuimarisha mtandao wa barabara ndani ya jiji la Arusha ukiunganisha maeneo mbalimbali muhimu ya Mbauda, kwa mrombo, barabara ya Bypass, Soko la Kilombero hadi Uwanja wa Ndege wa Kisongo hadi Uwanja wa AFCON.
Aidha, Ulega ametoa maelekezo kwa TANRAODS na Mkandarasi kuhakikisha wanatoa fursa za ajira kwa vijana hususani wa Mkoa wa Arusha wanaopitiwa na mradi kupitia ngazi ya ofisi ya Mkuu wa Wilaya ili mradi huo uweze kuwanufaisha kuongeza kipato na shughuli zao za kiuchumi.
Vilevile, Ulega amezitaka Taasisi za TANESCO na AUWASA kuharakisha kuhamisha miundombinu ya maji na umeme iliyopo katika barabara hiyo ili kuharikisha utekelezaji wake kwa urahisi na kwa ufanisi.
Kadhalika, Ulega ametoa rai kwa wananchii kuendelea kutoa ushirikiano kwa uongozi wa ngazi ya Wilaya, timu ya wataalam na mkandarasi na ili kazi ziende kwa haraka.
Naye, Mbunge wa Jimbo la Arusha, ambaye pia ni Waziri wa Habari, Utamaduni Sanaa na Michezo Paul Makonda ameeleza kuwa Arusha mpya yenye miundombinu bora inakuja chini ya Rais Dkt Samia Suluhu Hassan na hii inaonesha dhahiri kila kona unapokwenda katika Mkoa huu barabara zinajengwa.
Kwa upande wake, Meneja wa TANROADS mkoa wa Arusha, Mhandisi Reginald Masawe amesema kuwa mkataba wa mradi huo wenye thamani ya Shilingi Bilioni 221 ulianza kutekelezwa Aprili 10, 2026 baada ya Mkandarasi kulipwa malipo na kupewa kibali cha kuanza kazi na unatarajiwa kukamilika Machi 25, 2029
Ameeleza kuwa barabara hiyo itajengwa kwa kiwango cha kisasa, ikiwa na njia za watembea kwa miguu, mifereji ya kisasa ya maji pamoja na taa za barabarani.

