NA EMMANUEL MBATILO, CHATO.
Hayati Dkt.John Pombe Magufuli atakumbukwa kwa mengi hasa katika utendaji kazi wake kwani alikuwa hodari kuanzia alipokuwa Waziri mpaka alivyokuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Ameyasema hayo leo Rais Mstaafu wa awamu ya Nne Mhe.Dkt.Jakaya Mrisho Kikwete katika tukio la kutoa heshima za mwisho kwa mwili wa hayati John Pombe Magufuli wilayani Chato mkoani Geita.
Akizungumza katika tukio hilo Mhe.Dkt.Kikwete amesema Magufuli alikuwa ni mmoja wa Mawaziri aliowaamini na kuwatumaini ndio maana alimuweka kwenye Wizara tatu zilizokuwa ngumu.
“Nilipokuwa Rais, Magufuli alikuwa ni mmoja wa mawaziri niliowaamini na kuwatumaini, alikuwa jembe langu. Ndio maana nilimuweka kwenye wizara tatu zilizokuwa ngumu ili anyooshe mambo”.Mhe.Dkt. Kikwete.
Aidha Mhe.Dkt.Kikwete amesema katika mchakato wa kupitisha majina ya wagombea Urais 2015 hakuweza kusita kulichagua jina la Magufuli kwani alifahamu fika utendaji kazi.
Amesema alishangazwa na maneno yaliyokuwa yanasemwa kuwa hampendi Magufuli kwani Magufuli ni mmoja wa viongozi ambao ambao alikuwa hana mashaka nae katika utendaji kazi wake.
“Akutukanae hakuchagulii tusi, kuna mengi yamesemwa, mara ooh.. JK hampendi Magufuli, jamani mimi ndiye nilimkabidhi ilani ya Uchaguzi labda JK mwingine”. Amesema Mhe.Dkt.Jakaya Kikwete.