Home Mchanganyiko ULINZI WA NCHI NA MIPAKA YAKE NI SALAMA-CDF MABEYO

ULINZI WA NCHI NA MIPAKA YAKE NI SALAMA-CDF MABEYO

0

………………………………………………………………………….

Na.Alex Sonna,Chato

Mkuu wa Majeshi  nchini Tanzania (CDF) Venance Mabeyo amesema kuwa ulinzi wa nchi na mipaka yake ni salama na vyombo vitaendelea kukulinda kama Rais, kukutii kama amiri jeshi mkuu na kutekeleza majukumu yetu kama ilivyoainishwa kwenye Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Hayo ameyasema leo Machi 26,2021 wilayani Chato Mkoani Geita kwa niaba ya Wakuuu wa vyombo vya ulinzi na usalama wakati wa Ibada ya Mazishi ya Hayati Dkt.John Magufuli,Mabeyo amesema kuwa  hali ya nchi ni shwari na wataendelea kuimarisha ulinzi.

CDF Mabeyo amesema kuwa vyombo hivyo vitaendelea kuonyesha uadilifu, utiifu na uaminifu kwake kama ilivyokuwa kwa awamu za uongozi zilizopita.

“Vyombo vya ulinzi na usalama vinapenda kukuhakikishia kuwa ulinzi wa nchi na mipaka yake ni salama na vitaendelea kukulinda wewe, kukutii na kutekeleza majukumu yake aidha vinakuhakikishia utiifu, uadilifu na uaminifu mkubwa kwako” amesema CDF Mabeyo

Mabeyo amesema kuwa tangu aingie madarakani mwaka 2015 Hayati Dkt. John Magufuli, alionesha kuviamini na kuvipenda vyombo vya ulinzi na usalama kwa dhati kubwa, alihakikisha kuwa anaviwezesha kwa mahitaji ya kiutendaji na kiutawala ili viweze kutekeleza majukumu yake.
“Upendo wake kwa vyombo vya ulinzi na usalama aliuonesha kwa namna ambavyo alivishirikisha katika shughuli mbalimbali za kiuchumi na maendeleo ya nchi yetu, alisema hatuwezi kuwa na vyombo imara bila kuwa na uchumi madhubuti”amesema Mabeyo
Hata hivyo amesema kuwa Vyombo vya ulizni vilishirikishwa katika shughuli zote za kiuchumi mifano michache ni ushiriki wetu wa kuulinda mgodi wa Tanzanite, kabla ya kuulinda lakini tulijenga ukuta kuzunguka mgodi huo pia katika kujenga uchumi ambapo aliwekeza kwenye miradi ya kimkakati na kuweka miundombinu bora.

Aidha Mabeyo amemuomba Rais Samia kuwatunuku nishani askari wanafunzi waliotakiwa kutunikiwa nishani hizo Machi 10, 2021 na Hayati Rais Magufuli

”Hayati Magufuli alitakiwa awatunuku  nishani Februari 20 lakini kutokana na kazi zake tukasogeza mbele hadi Machi 6,alipomaliza ziara yake Dar es Salaam akaniambia hajisikii vizuri hivyo akaomba tusogeze hadi Machi 10 ili ajitazamie afya yake,” amesema Mabeyo

Aidha CDF Mabeyo amesema kuwa  Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mh. Samia Suluhu Hassan ataitwa pia Amiri Jeshi Mkuu wa Tanzania na sio Amirat kama ambavyo ilipendekezwa,“Nashukuru Baraza la Kiswahili limerekebisha uendelee kuitwa Amiri Jeshi Mkuu na sio Amirat kama ilivyokuwa inapendekezwa”

Mwili wa Hayati Dkt.John Magufuli unatarajiwa kupumzishwa leo katika nyumba ya milele alipozikwa Baba yake Mzazi.