NA DENIS MLOWE IRINGA
DIWANI wa Viti Maalum Kanda ya Kihesa Sara Ponela, amekabidhi mradi wa biashara ya magogo wenye thamani ya takribani shilingi milioni moja kwa wanawake wa Umoja wa Wanawake wa Chama Cha Mapinduzi (UWT) Kata ya Isakalilo, ukiwa na lengo la kuwawezesha wanawake kujikwamua kiuchumi na kuongeza ushiriki wao katika shughuli za maendeleo.
Akizungumza wakati wa makabidhiano yaliyofanyika katika Soko la Zizi la Ng’ombe, Ponela alisema mradi huo umetokana na maono ya kuwasaidia wanawake kupata chanzo cha uhakika cha mapato huku ukiwaandaa kunufaika na mikopo ya asilimia 10 inayotolewa na halmashauri kwa wanawake, vijana na watu wenye ulemavu.
Alisema moja ya masharti muhimu ya kupata mikopo hiyo ni kuwa na mradi unaoonekana na unaofanya kazi, jambo lililowasukuma kuanzisha biashara hiyo ya magogo na kuni kwa wanawake wa UWT Isakalilo.
“Tumewaza kuwasaidia wanawake hawa waweze kufanya biashara na kujitegemea kiuchumi lakini pia tumetazama mbele zaidi ili waweze kuwa na sifa za kupata mikopo inayotolewa na serikali kwa wanawake,” alisema Ponela.
Aliongeza kuwa mradi huo una fursa kubwa ya soko kutokana na mahitaji ya kuni na magogo katika shughuli mbalimbali ikiwemo uchomaji wa matofali, matumizi ya shule na kaya za wananchi.
Ponela aliwataka wanawake wengine kujitokeza kujiunga na vikundi vya maendeleo na UWT ili waweze kunufaika na fursa mbalimbali za kiuchumi zinazopatikana katika jamii.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa UWT Kata ya Isakalilo, Agnes Sanga, alimshukuru diwani huyo kwa kuanzisha mradi huo ambao alisema utawasaidia wanawake zaidi ya 70 waliopo kwenye umoja huo kujijengea uwezo wa kufanya biashara na kuimarisha maisha ya familia zao.
Alisema mradi huo utakuwa chachu kwa wanawake wengi waliokuwa na hofu ya kuanza biashara, huku akiwahimiza wanawake kujitegemea badala ya kutegemea kipato cha waume zao pekee.
“Tunamshukuru sana kwa kutuunga mkono mradi huu utatusaidia kujikwamua kiuchumi na kutuwezesha kuanzisha shughuli nyingine za maendeleo,” alisema Sanga.
Naye Katibu wa UWT Kata ya Isakalilo, Maneno Msigwa, alisema tangu kuingia madarakani hawakuwahi kupata mradi kama huo, akibainisha kuwa utaisaidia UWT kata hiyo kupata mapato yatakayorahisisha utekelezaji wa shughuli mbalimbali za chama na maendeleo ya wanachama.
Msigwa alisema wanachama 72 kutoka matawi sita ya UWT katika kata hiyo watanufaika na mradi huo, huku akiahidi kuwa watausimamia kwa uadilifu ili uwe endelevu na wenye manufaa kwa kizazi cha sasa na kijacho.
Akizungumza katika hafla hiyo, Diwani Mstaafu wa Kata ya Ilala, Conrad Mlowe, alimpongeza Sara Ponela kwa hatua hiyo akisema amekuwa mfano bora unaostahili kuigwa na madiwani wengine wa viti maalum nchini.
Alisema kuwapatia wananchi miradi ya maendeleo ni jambo lenye tija zaidi kuliko kuwapa fedha za matumizi ya muda mfupi, kwani miradi huendelea kuwanufaisha kwa muda mrefu na kuwawezesha kujitegemea.
Mlowe aliwataka madiwani wengine wa UWT kuiga mfano huo kwa kuanzisha miradi katika maeneo wanayoyalea ili kuongeza uwezo wa wanawake kushiriki kikamilifu katika shughuli za kiuchumi na maendeleo ya jamii.

