NA MWAMVUA MWINYI, CHALINZE
MBUNGE wa Jimbo la Chalinze, Ridhiwani Kikwete ametoa msaada wa vifaa mbalimbali ikiwemo mifuko ya saruji 20 na matofali 3,000 kwa ajili ya uanzishwaji ujenzi wa shule ya msingi katika kitongoji cha Choza .
Aidha amemkabidhi msaada wa baiskeli ya miguu mitatu (wheel Chair),mkazi wa Zomozi-Ubena mzee Cosmas Alphonce Chongwe ambae ni mlemavu wa miguu.
Katika hatua nyingine ,Ridhiwani alitoa fimbo nne maalum kwa ajili ya walemavu wa macho,kadi 23 za afya kwa ajili ya matibabu ya wazee, vyote vikiwa na thamani zaidi ya sh.milioni tano.
Mbunge huyo alitoa misaada hiyo baada ya kumaliza kikao chake alichofanya pamoja na wajumbe wa mkutano mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) kata ya Ubena-Zomozi.
Ridhiwani alieleza, msaada huo alitoutoa, ni sehemu ya utekelezaji wa ahadi za Ilani ya uchaguzi na maombi mbalimbali ya wananchi katika kata hiyo.
Pamoja na hayo, alikutana na wanachama mbalimbali wa vikundi vya maendeleo katika kata hiyo, ambapo aliwahimiza kuendelea kujiunga vikundi ili kuweza kupata mikopo kirahisi na kuwezeshwa kuliko kuwa mmoja mmoja.
Hakusita kusema, ataendelea kusaidia makundi maalum na kusimamia kero zinazowakabili wananchi wa jimbo la Chalinze.