Home Mchanganyiko WAZIRI AWESO AZITAKA MAMLAKA ZA MAJI KUELIMISHA WATEJA KUHUSU BEI ZA MAJISAFI

WAZIRI AWESO AZITAKA MAMLAKA ZA MAJI KUELIMISHA WATEJA KUHUSU BEI ZA MAJISAFI

0

Naibu Waziri wa Maji Mhe. Jumaa Aweso (Mb), mwenye shati la kitenge,  akikagua Dira inayoonyesha kiwango cha uzalishaji majisafi katika mtambo wa kusafisha maji wa Nyankanga, Geita. Maji yanayozalishwa ni lita laki mbili kwa saa, na yanahudumia wakazi wa mji wa Geita.

Naibu Waziri wa Maji Mhe. Jumaa Aweso (Mb), mwenye shati la kitenge,  akizindua jengo la Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Mjini Geita (GEUWASA). Hatua hiyo ni moja ya mikakati katika kuhakikisha wananchi wanapata huduma bora za maji na watumishi kufanya kazi katika mazingira yatakayowawezesha kutoa huduma bora zaidi kwa wateja.

Naibu Waziri wa Maji Mhe. Jumaa Aweso (Mb) akimuuliza akiuliza kwa  mwakilishi wa kampuni ya PET iliyopewa kandarasi ya mradi wa maji wa Nyamtukuza Bw. Bahati Mwaipopo  (kulia-tshirt ya mistari) kuhusu utekelezaji wa mradi huo, toka kuanza mwaka 2014 wananchi hawajapata maji. Bw. Mwaipopo ametakiwa kutoa maelezo Polisi.

Naibu Waziri wa Maji Mhe. Jumaa Aweso (Mb) akiongea na wananchi wa Nyang’hwale kuhusu mradi wa maji wa Nyamtukuza ulioanza kutekelezwa mwaka 2014. Waziri Aweso amewataka wataalam wa mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Jijini Mwanza (MWAUWASA) na Mamlaka ya Maji Geita (GEUWASA), pamoja na mtalaam wa maji kutoka Wizara ya Maji kufanya kazi ambazo hazihitaji kandarasi kwa pamoja  ili wananchi wapate huduma ya maji mapema.

Sehemu ya wakazi wa Nyang’wale wakimsikiliza Naibu Waziri wa Maji Mhe. Jumaa Aweso (Mb) katika uwanja wa Kharumwa. Wakazi hao walitumia fursa ya kikao hicho kuwasilisha kero mbalimbali ikiwamo mradi wa maji wa Nyamtukuza ambao umechukua muda kukamilika. Hata hivyo, wataalam wa Wizara ya Maji wametumwa kuongeza nguvu ili wananchi hao waanze kupata maji.

…………………………………………….

Wakati Serikali inalo jukumu la kuhakikisha wananchi wanapata huduma ya majisafi, salama na yenye kutosheleza, wananchi nao wanapaswa kutimiza wajibu kwa kulipia huduma hiyo kadri wanavyotumia maji kama walivyokubaliana na mamlaka zinazotoa huduma katika maeneo yao.

Naibu Waziri wa Maji Mhe. Jumaa Aweso (Mb) amesema hayo wakati akizindua jengo la Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Mjini Geita (GEUWASA) lililopo katika kata ya Kalangalala, mjini Geita.

Mhe. Aweso amesema bei ya maji huidhinishwa na Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA), baada ya utaratibu maalumu kufanyika, ikiwamo kuwashirikisha wadau wote katika vikao vya mapendekezo ya bei. Amefafanua kuwa huduma ya majisafi na salama inahitajika zaidi na kuna gharama zake, ikiwamo umeme na dawa za kutibu maji.

Mhe. Aweso ameitaka GEUWASA kutoa elimu ya kutosha kwa wananchi na wateja wake kuhusu mabadiliko ya bei za maji yaliyofanyika hivi karibuni, ili waweze kutoa ushirikiano wa kutosha na kuiwezesha mamlaka hiyo kujiimarisha kwa kuongeza mtandao wa majisafi katika maeneo ambayo hayajafikiwa, ikiwamo Nyanguku na Ihanamilwa. Mabadiliko hayo ya bei ya maji ya GEUWASA yalitangazwa katika Gazeti la Serikali Namba 193 la tarehe 3 Mei, 2019.

Wakati huohuo, Mhe. Aweso (Mb) akiongea na wananchi wilayani Nyang’hwale katika uwanja wa Kharumwa amemtaka mwakilishi wa kampuni ya Pet, iliyopewa kandarasi ya mradi wa maji wa Nyamtukuza kutoa maelezo Polisi kwa kuchelewesha mradi wakati Serikali imelipa fedha. Aidha, ili kuhakikisha mradi huo ulioanza Januari 2014 unakamilika haraka, Waziri Aweso (Mb) ameitaka Mamlaka ya Majisafi Jijini Mwanza (MWAUWASA) na ile ya Geita (GEUWASA), pamoja na mtaalam mmoja wa maji kutoka Wizara ya Maji kufika katika mradi huo na kufanya kazi ambazo hazihitaji kutoa kandarasi.