VIJANA Maalum wa UVCCM Mkoa wa Kusini Unguja wakiwa wamebeba Jeneza la aliyekuwa Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM Taifa Marehemu Ramadhan Abdallah Shaaban kwa ajili ya Mazishi yake yaliyoongozwa na Mjumbe wa Kamati Kuu ya CCM Taifa Balozi Seif Ali Idd yaliyofanyika leo Kijijini kwako Uzini Wilaya ya Kati Mkoa wa Kusini Unguja.
Mjumbe wa Kamati Kuu ya CCM Taifa ambaye pia ni Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Idd akiongoza mazishi kwa kuweka udongo katika Kaburi la aliyekuwa Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM Taifa Marehemu Ramadhan Abdallah Shaaban aliyefariki jana akiwa katika Matibabu katika Hospitali ya Agakhan Jijini Dar es saalam.
NAIBU Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar Dk.Abdulla Juma Mabodi akiweka udongo katika Kaburi la Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM Taifa Marehemu Ramadhan AbdallaH Shaaban aliyefariki jana akiwa katika Matibabu katika Hospitali ya Agakhan Jijini Dar es saalam.
………………………………………………
NA IS-HAKA OMAR,ZANZIBAR.
MJUMBE wa Kamati Kuu ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) Taifa ambaye pia ni Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Idd, leo ameongoza Maelfu ya Wananchi katika Mazishi ya Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM Taifa Marehemu Ramadhan Abdallah Shaaban aliyefariki akiwa katika Matibabu huko katika Hospitali ya Agakhan Jijini Dar es saalam na amezikwa leo kijijini kwao Uzini Wilaya ya Kati Mkoa wa Kusini Unguja.
Mazishi hayo yameudhuriwa na Viongozi Watendaji wa CCM na Serikali pamoja na Wana CCM na Wananchi kwa ujumla.
Viongozi walioudhuria mazishi hayo ni pamoja na Naibu Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar Dk.Abdulla Juma Saadalla,Spika wa Baraza la Wawakilishi Zanzibar Mhe.Zubeir Ali Maulid na Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamy wa Pili wa Rais Aboud Mohamed Aboud.
Wengine ni Wajumbe wa Kamati Kuu ya CCM Taifa, Wajumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM Taifa, Mawaziri na Manaibu Mawaziri, Wabunge na Wawakilishi,Wakurugenzi wa Idara mbali mbali za SMZ,Wenyeviti na Makatibu wa CCM wa ngazi mbali mbali pamoja na Wana CCM na Wananchi.
Katibu wa CCM Mkoa wa Kusini Unguja Suleiman Mzee Suleiman, akisoma wasifu wa marehemu amesema CCM imepokea kwa mshtuko na masikitiko makubwa taarifa ya Kifo cha Ramadhan Abdallah Shaaban ambaye alikuwa ni Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM Taifa kutoka Mkoa wa Kusini Unguja na Mkurugenzo wa Uratibu wa Uchaguzi Afisi Kuu ya CCM Zanzibar.
Amesema Marehemu Ramadhan Abdalla Shaaban alizaliwa mwaka 1948 katika Mkoa wa Kusini Unguja Wilaya ya Kati katika Kijiji cha Uzini na kupata Elimu yake ya Msingi kuanzia mwaka 1964 hadi 1967 katika Skuli ya Msingi Ndijani Wilayani humo.
Pia alieleza kwamba Marehemu aliendelea na Elimu yake ya Sekondari katika Skuli ya Sekondari ya Lumumba mwaka 1968 hadi 1976 alipomaliza Kidato cha Nne na kujiunga na Chuo cha Ualimu cha Nkuruma na kuhitimu Diploma ya Ualimu, na kujiendeleza kielimu katika Vyuo Vikuu mbali mbali vya ndani na nje ya Nchi.
Kupitia risala hiyo imeeleza kuwa Marehemu enzi za uhai wake alikuwa Mwanachama na Kiongozi Mtiifu wa kuaminika lakini pia alikuwa Mshauri ,Mkufunzi na mpiganaji na kamanda mzuri aliyelinda maslahi ya CCM na Muumini mzuri wa Siasa ya Ujamaa na Kujitegemea.
Katika maelezo yake Katibu huyo, ameeleza kuwa Marehemu Enzi za Uhai wake aliwahi kushika nyadhifa mbali mbali katika Chama na Serikali ambapo alikuwa ni miongoni mwa Makada Watiifu wa Afro-Shirazi Party Yourth Legue na Mwanachama wa ASP.
Alisema mwaka 1977 alikuwa ni Balozi na Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM Tawi la Uzini, Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM Wilaya ya Kati na mwaka 1980 alichaguliwa kuwa Mjumbe wa Baraza la Wawakilishi na kuwa Waziri wa Biashara Zanzibar.
Nyadhifa nyingine alizowahi kushika Marehemu Ramadhan enzi za uhai wake mwaka 1980 hadi 1985 alikuwa Mbunge na Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Muungano katika Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, mwaka 1988 alichaguliwa kuwa Mjumbe wa Baraza Kuu la JUWATA Tanzania.
Mnamo mwaka 2005 hadi 2015 tena kuwa Mjumbe wa Baraza la Wawakilishi na Waziri katika Wizara mbali mbali za SMZ zikiwemo Waziri wa Katiba na Sheria, Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali pamoja na Waziri wa Ardhi, Nyumba,Maji na Nishati na hadi kifo chake alikuwa Mjumbe wa NEC CCM Taifa na Mkurugenzi wa Uratibu wa Uchaguzi wa Afisi Kuu ya CCM Zanzibar.
Sambamba na hayo Katibu huyo alieleza kuwa Marehemu Ramadhan ataendelea kukumbukwa kwa Mchango wake Mkubwa katika uhai wake ndani ya CCM na Serikali zote mbili ya Zanzibar na Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Fikra zake zitaenziwa kwa Vitendo katika mapambano ya Siasa za Ujamaa na Kujitegemea.
Marehemu ameacha Vizuka wawili na Watoto Tisa.
Mwenyezi Mungu ailaze roho ya Marehemu mahala Pema Peponi Amin.