Mashindano ya Rhino Cup yamefikia tamati leo tarehe 8 oktoba, 2026 kwa timu ya kata ya Olbalbal kuicharaza bila huruma jumla ya Goli 3-2 timu ya Nainokanoka katika mchezo wa fainali uliochezwa uwanja wa Makao Kata ya Ngorongoro mkoani Arusha.

Katika mchezo wa kutafuta mshindi wa 3 timu ya kata ya Endelen imeibamiza kata ya Ngoile kwa goli 2-1 huku mchezo ukiwa umetawaliwa na mbinu na ufundi uliokuwa ukishuhudiwa na Twiga, Ngiri, pundamilia na nyati waliokuwa pembezoni mwa uwanja.

Akikabidhi kikombe cha ushindi kwa niaba ya Kamishna wa Uhifadhi, Meneja wa Idara ya maendeleo ya Jamii SACC Gloria Bideberi ameipongeza timu ya Olnalbal na kueleza kuwa mashindano ya Rhino Cup yamelenga kuibua vipaji vya michezo, kuhamasisha shughuli za uhifadhi na kuboresha uhusiano kati ya mamlaka na jamii ya wananchi wanaoishi hifadhi ya Ngorongoro.

Bingwa wa mashindano hayo amekabidhiwa Kombe, fedha taslimu na kupewa safari ya kwenda kushuhudia mtanange wa Simba na Yanga tarehe 10 Oktoba, 2026 Jijini Dar es Salaam.