Na Meleka Kulwa – Fullshangwe Blog, Dodoma
Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Balozi Dkt. Bashiru Ali Kakurwa, amesema thamani ya mifugo nchini imeongezeka kutoka Sh. trilioni 26.57 mwaka 2020/2021 hadi Sh. trilioni 33.22 mwaka 2024/2025.
Akizungumza katika kilele cha Maadhimisho ya Sikukuu ya Wakulima Nanenane yaliyofanyika katika Viwanja vya Maonesho vya Dkt. John Samuel Malecela jijini Dodoma, Balozi Dkt. Bashiru amesema ongezeko hilo ni miongoni mwa mafanikio yaliyopatikana kutokana na utekelezaji wa majukumu ya Wizara ya Mifugo na Uvuvi.
Amebainisha kuwa idadi ya mifugo nayo imeendelea kuongezeka, ambapo ng’ombe wameongezeka kutoka milioni 39.2 hadi milioni 40.57, huku mbuzi wakiongezeka kutoka milioni 28.59 hadi milioni 29.99.
Aidha, amesema idadi ya kondoo imeongezeka kutoka milioni 9.67, huku akibainisha kuwa ongezeko la mifugo ni sehemu ya mafanikio yaliyopatikana katika kipindi hicho.
Pia amemshukuru na kumpongeza Waziri Mkuu Dkt. Mwigulu Nchemba kwa kuzindua Mkakati wa Ufugaji wa Kuku wa Miaka 10 katika viwanja hivyo tarehe 1 Agosti 2026, akibainisha Kuwa mkakati huo umetokana na maelekezo ya Serikali na una umuhimu mkubwa katika maisha ya kiuchumi ya wananchi.
Aidha, amesema eneo lingine ambalo limekuwa na mafanikio ni upatikanaji wa maeneo ya malisho, ambapo Wizara ya Mifugo na Uvuvi kwa kushirikiana na Tume ya Taifa ya Mipango ya Matumizi ya Ardhi imeandaa mipango ya matumizi ya ardhi inayowezesha kutenga maeneo kwa ajili ya malisho.
Amebainisha kuwa hadi mwaka 2025/2026, ardhi iliyotengwa kwa ajili ya malisho imefikia hekta milioni 3.69, kutoka hekta milioni 3.49 mwaka 2024/2025.
Ameongeza kuwa hadi kufikia Aprili 2026, hekta milioni 1.35 katika vijiji 365 zimepimwa na kutangazwa kwenye Gazeti la Serikali.
