Mkuu wa kanda wa COPRA,Fahmia Selemani akizungumza na waandishi wa habari kwenye maonesho ya nanenane Njiro
………….
Na Happy Lazaro, Arusha
Mamlaka ya Udhibiti wa Nafaka na Mazao Mchanganyiko (COPRA) imesema inasimamia takribani mazao 120 yaliyogawanyika katika makundi matano makuu, huku ikisisitiza kuwa jukumu lake ni kuhakikisha uzalishaji, biashara na usafirishaji wa mazao hayo unazingatia viwango vya ubora vinavyokubalika ndani na nje ya nchi.
Akizungumza katika maonesho ya Nanenane Kanda ya Kaskazini, Mkuu wa kanda wa COPRA,Fahmia Selemani amesema mazao yanayosimamiwa na mamlaka hiyo yamegawanywa katika makundi ya nafaka, mikunde, mazao ya bustani, mazao ya mizizi pamoja na mazao ya mafuta.
Amefafanua kuwa kundi la nafaka linajumuisha mazao kama mahindi, mpunga, ngano, ulezi na uwele, huku kundi la mikunde likihusisha maharage, soya, choroko, dengu na mazao mengine ya jamii hiyo.
Kwa upande wa mazao ya bustani, amesema COPRA inasimamia matunda mbalimbali ikiwemo parachichi, ambalo ni zao la kimkakati linalochangia kwa kiasi kikubwa mapato ya taifa kupitia mauzo ya nje.
Fahamia ameongeza kuwa ,mamlaka hiyo imeweka kanuni za ubora pamoja na miongozo ya uzalishaji na masoko ili kuhakikisha wakulima na wanunuzi wanafuata taratibu zinazotakiwa.
Fahmia amefafanua kuwa kundi la mazao ya bustani pia linajumuisha viungo kama iliki, pilipili manga, mdalasini, karafuu, manjano na tangawizi, ambavyo huuzwa kupitia mifumo rasmi ya biashara inayosimamiwa na COPRA. Pia mamlaka hiyo inasimamia mazao ya maua na pareto.
Ameongeza kuwa kundi la mazao ya mizizi linahusisha mihogo, magimbi, viazi vitamu na viazi mviringo, wakati kundi la mazao ya mafuta linajumuisha alizeti, ufuta, karanga, soya na michikichi.
“kutokana na idadi kubwa ya mazao yanayosimamiwa, COPRA inahudumia wadau wengi katika mnyororo mzima wa thamani kuanzia uzalishaji, ukusanyaji, biashara, usafirishaji hadi masoko ya ndani na nje ya nchi. Hivyo, aliwahimiza wadau kuzingatia sheria, viwango vya ubora na kujisajili katika mifumo rasmi ili kuongeza ushindani wa mazao ya Tanzania katika soko la kimataifa.”amesema Fahmia .
Amebainisha kuwa kaulimbiu ya COPRA ni “Shirikisha, Boresha, Endeleza,” inayolenga kuimarisha ushirikiano kati ya wadau wote wa sekta ya mazao kwa ajili ya kuongeza tija, ubora na fursa za kibiashara.
“dhamira yetu ni kuchochea mageuzi ya mnyororo wa thamani wa nafaka na mazao mchanganyiko kwa kuimarisha viwango endelevu vya uzalishaji,kukuza uchakataji wa mazao ya kilimo,na kuwezesha upatikanaji wa masoko yenye faida ili kuongeza ushindani na kuimarisha usalama wa chakula.”amesema .
Aidha Fahmia amewataka wakulima nchini kutembelea banda lake ili kupata elimu kuhusu huduma mbalimbali zinazotolewa na mamlaka hiyo pamoja na kutambua fursa zilizopo katika masoko ya mazao ya kilimo.
Amesema kuwa,mazao ya kilimo siyo kwa ajili ya chakula pekee, bali pia ni bidhaa za biashara zinazoweza kumsaidia mkulima kuongeza kipato na kuboresha maisha yake.
Amefafanua kuwa, kupitia banda la COPRA wakulima wanapata fursa ya kujifunza namna bora ya kuzalisha mazao yenye ubora unaokidhi mahitaji ya soko la ndani na la kimataifa, pamoja na kufahamu aina ya mazao yenye uhitaji mkubwa sokoni.
“Tunawakumbusha wakulima kuwa kilimo ni biashara. Mazao tunayozalisha tunatumia kwa ajili ya lishe, lakini pia yana thamani ya kiuchumi kwa sababu yanaweza kuuzwa na kumpatia mkulima kipato,” amesema Fahmia .
Aidha, amewataka wakulima kutumia fursa zinazopatikana nchini, akieleza kuwa Tanzania ina ardhi kubwa yenye rutuba inayowezesha uzalishaji wa mazao mbalimbali kwa ajili ya matumizi ya ndani na biashara ya kimataifa.
Amesisitiza kuwa uwepo wa sera wezeshi za Serikali unalenga kuwawezesha wakulima kuzalisha kwa tija, kupata masoko na hatimaye kupata faida kupitia shughuli zao za kilimo.
Aidha ametoa wito kwa wakulima kufika kwenye banda lake ili kupata elimu na taarifa zitakazowawezesha kufanya kilimo chenye tija na chenye kuleta mafanikio kiuchumi.

