Na Meleka Kulwa – Fullshangwe Blog, Dodoma

Waziri wa Kilimo, Mhe. Daniel Chongolo, amesema Serikali imefikia hatua ya kuanza utekelezaji wa masoko ya kimkakati kwa ajili ya biashara ya mazao ambayo hayajawekewa utaratibu, ikiwemo mahindi na mpunga.

Ameyasema hayo Agosti 8, 2026, wakati wa kilele cha Maonesho ya Nane Nane kitaifa katika Viwanja vya Dkt. John Samuel Malecela vilivyopo Nzuguni, Jijini Dodoma, ambapo amebainisha kuwa Serikali tayari imetambua maeneo manne ya kuanzia utekelezaji wa mpango huo ambayo ni Ruvuma, Njombe, Songwe na Rukwa.

Amesema maeneo hayo yamechaguliwa kwa kuwa ni miongoni mwa mikoa inayozalisha kwa wingi mpunga na mahindi, huku akieleza kuwa lengo ni kujenga silos pamoja na maghala yatakayowezesha kuhifadhi tani 150,000 za nafaka kwa wakati mmoja.

Ameongeza kuwa mpango huo unalenga kuimarisha soko, kupunguza upotevu wa mazao baada ya kuvuna na kupunguza changamoto ya sumukuvu, huku ukisaidia Serikali kuwa na udhibiti wa biashara ya mazao nchini.

Aidha, amesema hatua hiyo inalenga kudhibiti wafanyabiashara kutoka mataifa mengine ambao wamekuwa wakiingia nchini na kwenda moja kwa moja mashambani kununua mazao kutoka kwa wakulima, hali ambayo amesema imekuwa ikifanya Serikali kukosa udhibiti wa biashara hiyo.

Amesema vituo hivyo vitafanya kazi kama masoko ya kitaifa na kimataifa ya mazao na vitasaidia kuratibu na kudhibiti uuzaji wa mazao, hususan kwa wafanyabiashara wanaotoka nje ya nchi.

Amebainisha kuwa katika kuwawezesha vijana na wanawake kupata mitaji, Serikali imetoa mikopo yenye thamani ya Sh. bilioni 76 yenye riba isiyozidi asilimia 9 kwa vijana na wanawake 2,366 kupitia Benki ya Ushirika kwa kushirikiana na Mfuko wa Udhamini wa Pembejeo za Kilimo (AGITF).

Aidha, amesema Serikali imeanza kutekeleza programu ya Jenga Kesho Iliyo Bora (BBT) katika halmashauri 18 nchini, baada ya mradi wa awali wa majaribio katika vituo vya Chinangali na Ndogowe kufanikiwa na kuonyesha namna vijana walivyohamasika kushiriki katika kilimo.

Amesema katika halmashauri hizo, jumla ya hekta 126,180.75 zinaendelea kuandaliwa kwa ajili ya kuanza uzalishaji.

Juu ya mafuta ya kula, amebainisha Kuwa Serikali imepitisha kanuni inayowataka wachakataji na waagizaji wa mafuta kutoka nje ya nchi kuwa na mashamba ya kuzalisha mazao ya mbegu za mafuta, ikiwemo alizeti na chikichi, pamoja na kuwa na kiwanda cha kuchakata mafuta ya kula.

Amesema hatua hiyo imechukuliwa kutokana na Tanzania kuwa na upungufu wa mafuta ya kula, ambapo kwa mwaka uzalishaji ni tani 306,000 dhidi ya mahitaji ya tani 732,000, hali inayolazimisha nchi kuagiza zaidi ya tani 426,000 za mafuta kwa mwaka kwa kutumia zaidi ya dola milioni 300.

Huku akibainisha kuwa Wakala wa Taifa wa Huduma za Ugani Kilimo (NAESA) utafanya kazi kwa karibu na wizara za kisera, sekretarieti za mikoa, mamlaka za serikali za mitaa na wadau wengine wa sekta ya umma na binafsi ili kuongeza ufanisi na kuchangia kufikia malengo ya kitaifa.

Pia, amebainisha kuwa Maonesho ya Nane Nane ya mwaka huu yamewashirikisha waonyeshaji 1,168, wakiwemo waonyeshaji 25 kutoka nchi za nje, huku hadi saa 4:00 asubuhi wakulima, wafugaji, wavuvi na wananchi 282,206 wakiwa wameshiriki katika maonyesho hayo.