Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya linawashikilia, David Mwakalinga [63] na Sarah Ngama [52] ambao ni mume na mke wote wakazi wa Mji Mwema -Lubele Wilayani Kyela kwa tuhuma za kumfanyia vitendo vya ukatili mtoto wao aitwaye Godliver Mwakalinga [17] mkazi wa Mji Mwema.

Tukio hilo lilibainika Agosti 7, 2026 maeneo ya Mji Mwema – Lubele, Kata ya Ikimba, Tarafa ya Unyakyusa, Wilaya ya Kyela, Mkoa wa Mbeya, inadaiwa kuwa baba mzazi wa mtoto huyo aitwaye David Mwakalinga [63] kwa kushirikiana na mama wa kambo wa mtoto huyo aitwaye Sarah Ngama [52] walimfunga mhanga mnyororo miguuni na kisha kubana kwa kufuli mbili na kumuweka ndani katika chumba cha peke yake.

Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya baada ya kupata taarifa za siri kutoka kwa raia wema lilianza ufuatiliaji na kufanikiwa kufika nyumbani kwa watuhumiwa na kukuta mhanga akiwa amefungwa mnyororo wenye kufuli mbili na kufungiwa katika chumba cha peke yake kwa madai kuwa ni kumdhibiti asitoroke kwa imani kuwa ana mapepo.

Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya linaendelea kutoa wito kwa baadhi ya wazazi na walezi wenye tabia ya kuwafanyia vitendo vya ukatili watoto kuacha mara moja kwani ni kinyume cha sheria na maadili, kwani Jeshi la Polisi halitasita kumchukulia hatua za kisheria yeyote atakayebainika kukiuka sheria na kufanya vitendo kama hivyo.