Waziri wa Fedha, Mhe. Balozi Khamis Mussa Omar (Mb) (kulia), akimkabidhi Funguo za Trekta kama Mkopo kutoka Benki ya CRDB, Mkazi wa Jiji la Mbeya, Bi. Christina Levi Mgaya (Katikati), kwa ajili ya kumwezesha katika shughuli zake za kuendeleza kilimo, wakati alipotembelea Mabanda ya Maonesho katika Viwanja vya John Mwakangale, jijini Mbeya kwa ajili ya kuhitimisha kilele cha Maadhimisho ya Siku ya Wakulima Duniani- Nane Nane, Kanda ya Nyanda za Juu Kusini. Jijini Mbeya.
Waziri wa Fedha, Mhe. Balozi Khamis Mussa Omar (Mb) (kulia), akisikiliza maelezo ya Afisa Maliasili Mkoa wa Mbeya, Bw. Petro Haule, kuhusu aina mbalimbali ya mavazi ya kale ambayo yalitokana na Ngozi, wakati alipotembelea Banda la Maliasili la Mkoa wa Mbeya, katika Viwanja vya John Mwakangale, jijini Mbeya ambapo alikuwa mgeni rasmi katika hafla yakuhitimisha kilele cha Maadhimisho ya Siku ya Wakulima Duniani- Nane Nane, Kanda ya Nyanda za Juu Kusini, jijini Mbeya. 
Waziri wa Fedha, Mhe. Balozi Khamis Mussa Omar (Mb) (kulia), akisikiliza maelezo ya Meneja Utafiti wa Kiwanda cha Mbolea cha INTRACOM, Dkt. Tulole Buchoyeke, kuhusu tafiti za mbolea wanazozalisha, wakati alipotembelea Mabanda ya maonesho, katika Viwanja vya John Mwakangale, jijini Mbeya ambapo alikuwa Mgeni Rasmi katika hafla ya kuhitimisha kilele cha Maadhimisho ya Siku ya Wakulima Duniani- Nane Nane, Kanda ya Nyanda za Juu Kusini, Jijini Mbeya. 
Waziri wa Fedha, Mhe. Balozi Khamis Mussa Omar (Mb) (kushoto) akiangalia moja ya bidhaa ya Siagi ya Karanga inayozalishwa na Mjasiliamali Mdogo kupitia Kampuni yake ya Swahigo Enterprises, Bw. Albert Thomas (kulia), wakati alipotembelea Mabanda ya Maonesho, katika Viwanja vya John Mwakangale, jijini Mbeya ambapo alikua Mgeni Rasmi katika hafla ya kuhitimisha kilele cha Maadhimisho ya Siku ya Wakulima Duniani – Nane Nane, Kanda ya Nyanda za Juu Kusini, Jijini Mbeya.
Waziri wa Fedha, Mhe. Balozi Khamis Mussa Omar (katikati) akiteta jambo na Mbunge wa Mbeya Mjini, Mhe. Patrick Mwalunenge (kushoto), wakati wakitembelea mabanda mbalimbali katika Viwanja vya John Mwakangale, jijini Mbeya ambapo alikua Mgeni Rasmi katika hafla ya kuhitimisha kilele cha Maadhimisho ya Siku ya Wakulima Duniani – Nane Nane, Kanda ya Nyanda za Juu Kusini, Jijini Mbeya. Kulia ni Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Mhe.. Beno Malisa.
(Picha na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini, WF, Mbeya)
…………….
Na Benny Mwaipaja, Mbeya
Serikali imetangaza kuendelea kuongeza uwekezaji mkubwa katika sekta za kilimo, mifugo na uvuvi, huku ikizitaka jamii za Nyanda za Juu Kusini kutumia fursa za soko, teknolojia na miundombinu ili kuongeza tija na kuharakisha utekelezaji wa malengo ya Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050.
Kauli hiyo ilitolewa mkoani Mbeya na Waziri wa Fedha, Mhe. Balozi Khamis Mussa Omar (Mb), wakati wa kilele cha Maonesho na Sherehe za Wakulima Nanenane Kanda ya Nyanda za Juu Kusini, yaliyofanyika katika Viwanja vya John Mwakangale, jijini Mbeya.
Akizungumza mbele ya viongozi wa serikali, wadau wa maendeleo, wakulima, wafugaji na wavuvi, Mhe. Balozi Omar alisema kaulimbiu ya Nanenane ya mwaka huu, “Tambua soko: Ongeza tija kutekeleza Dira ya 2050,” inapaswa kuwa chachu ya kuongeza uzalishaji wenye tija kuanzia shambani hadi kwenye masoko ya ndani na nje ya nchi.
Alisema uchumi wa Taifa umeendelea kuimarika, ambapo pato ghafi la Taifa lilifikia shilingi trilioni 234.1 mwaka 2025, kutoka shilingi trilioni 211.97 mwaka 2024, sawa na ukuaji wa asilimia 5.9 na Sekta ya kilimo nayo imeendelea kuonesha mafanikio makubwa, ikikua kwa asilimia 5.5 mwaka 2025 ikilinganishwa na asilimia 3.7 mwaka 2021, huku ikichangia asilimia 24.3 ya uchumi wa Taifa.
Kwa upande wa Kanda ya Nyanda za Juu Kusini, Mhe. Balozi Omar alisema eneo hilo limeendelea kuwa mhimili mkubwa wa uzalishaji na uchumi wa nchi. Alieleza kuwa pato la kanda hiyo lilifikia shilingi trilioni 32.8 mwaka 2024, sawa na asilimia 15.8 ya pato la Taifa, likiongezeka kutoka shilingi trilioni 29.6 mwaka 2023. Mkoa wa Mbeya uliongoza kwa pato la shilingi trilioni 11.6, ukifuatiwa na Iringa, Rukwa, Songwe, Njombe na Katavi.
Katika hatua ya kuimarisha sekta za uzalishaji, Mhe. Balozi Omar, alisema Serikali imeongeza bajeti ya sekta ya kilimo kutoka shilingi bilioni 276.72 mwaka 2021/22 hadi shilingi bilioni 1,132.36 mwaka 2026/27. Kati ya fedha hizo, shilingi bilioni 698.99 zitaelekezwa Wizara ya Kilimo na shilingi bilioni 433.38 Wizara ya Mifugo na Uvuvi.
Alisema pia kuwa Serikali imeidhinisha shilingi bilioni 384.29 kwa mwaka 2026/27 kwa ajili ya ujenzi na ukarabati wa miundombinu ya umwagiliaji nchini, hatua ambayo imechangia kuongezeka kwa eneo la umwagiliaji hadi hekta 983,466.1 mwaka 2025 kutoka hekta 727,280.6 mwaka 2022.
Akizungumzia hali ya chakula, Mhe. Balozi Omar alisema mikoa ya Nyanda za Juu Kusini imeendelea kufanya vizuri kwa kuwa na wastani wa uwezo wa kujitosheleza kwa chakula wa asilimia 219, juu zaidi ya kiwango cha chini kinachohitajika cha asilimia 120 na wastani wa Taifa wa asilimia 129.
Katika sekta ya mifugo na uvuvi, alisema Serikali imeendelea kuwekeza katika chanjo, masoko, mialo, boti za doria na usimamizi wa rasilimali za maji katika maziwa ya Nyasa, Rukwa na Tanganyika.
Aliongeza kuwa katika mikoa hiyo, jumla ya malambo 50 na mabwawa ya samaki 5,695 yamejengwa katika vipindi tofauti ili kuongeza uzalishaji na kipato kwa wananchi.
Kwa upande wa vijana, Mhe. Balozi Omar alisema Serikali imetenga shilingi bilioni 23 kupitia dirisha la mifugo na uvuvi kwa ajili ya kuwezesha miradi mbalimbali ya vijana, akisisitiza kuwa ushiriki wao ni muhimu katika kukuza uchumi wa sekta hizo.
Aliwataka viongozi wa mikoa na wilaya kusimamia amani, lishe, uhifadhi wa mazingira, pamoja na uanzishwaji wa vituo vya taarifa na teknolojia za kilimo katika kila kata ili kuwafikishia wakulima huduma na ubunifu unaooneshwa akisisitiza kuwa mafanikio ya sekta hizo yatategemea zaidi uzalishaji wenye tija, uhifadhi wa chakula, na matumizi bora ya fursa za soko.
