NA DENIS MLOWE ,IRINGA
WANANCHI wa Kata za Itunundu na Mboliboli, Tarafa ya Pawaga mkoani Iringa, wameeleza kufurahishwa na mafanikio ya Mradi wa Umwagiliaji wa Mkombozi wakisema umeongeza uzalishaji wa mpunga, kupunguza gharama za uzalishaji na kuondoa changamoto zilizokuwa zikiwakabili kwa miaka mingi.
Wakizungumza mbele ya Kamati ya Siasa ya CCM Mkoa wa Iringa iliyoongozwa na Mwenyekiti wa CCM Mkoa huo, Daud Yassin, wakati wa ziara ya kutembelea na kukagua maendeleo ya Mradi wa Umwagiliaji wa Mkombozi, wananchi hao walisema mradi huo umeleta mapinduzi makubwa katika shughuli za kilimo cha umwagiliaji kwa kuongeza uzalishaji, kupunguza gharama za uzalishaji na kuboresha maisha yao.
Mwenyekiti wa Skimu ya Mkombozi, Tachasco Simsamba, alisema kabla ya mradi huo wakulima walikuwa wanategemea mfereji wa asili ambao ulikuwa ukiharibika mara kwa mara, hasa wakati wa mvua kubwa, hali iliyowalazimu kutumia muda na fedha nyingi kurekebisha miundombinu ya muda ili kupata maji ya umwagiliaji.
Alisema hali hiyo imebadilika baada ya ujenzi wa mradi huo ambapo sasa maji yanafika mashambani kwa urahisi na shughuli za kilimo zinaendelea bila usumbufu mkubwa.
“Mradi huu umetukomboa kweli. Zamani tulikuwa tunahangaika kuweka vizuizi vya muda kwa kutumia miti na magunia ili kuelekeza maji mashambani, lakini sasa maji yanapatikana kwa kufungua mifereji tu tunamshukuru Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kutuletea mradi huu,” alisema Simsamba.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Ndete Store, Lucas John Ndete, alisema ongezeko la uzalishaji wa mpunga limewanufaisha pia wafanyabiashara na wasindikaji wa zao hilo.
Alisema kabla ya mradi huo alikuwa na ghala moja lenye uwezo wa kuhifadhi magunia 10,000 ya mpunga, lakini msimu huu baada ya kuanza kutumika kwa mradi huo ameweza kujaza maghala matatu yenye jumla ya takribani magunia 27,000.
“Tumeona mabadiliko makubwa. Uzalishaji umeongezeka sana na biashara yetu imepanuka. Tunamshukuru Rais pamoja na Serikali kwa kutekeleza mradi huu wenye manufaa makubwa kwa wakulima na wafanyabiashara,” alisema Ndete.
Mkazi wa Kijiji cha Mbuyuni na Mjumbe wa Kamati ya Halmashauri ya Kijiji hicho, Kipimo Chaukinga, alisema hapo awali wanaume walikuwa wakilazimika kukata miti na kujenga vizuizi vya muda mtoni ili kuelekeza maji kwenye mifereji ya umwagiliaji, jambo lililokuwa likiharibu mazingira na kuongeza ugumu wa kilimo.
Alisema baada ya kukamilika kwa sehemu kubwa ya mradi huo, wakulima sasa wanapata maji kwa urahisi, mavuno yameongezeka na uharibifu wa mazingira umepungua.
Akitoa taarifa ya maendeleo ya mradi huo, Meneja wa Tume ya Taifa ya Umwagiliaji (NIRC) Mkoa wa Iringa, Mhandisi Peter Akonaay, alisema mradi wa Skimu ya Mkombozi unatekelezwa katika kata za Itunundu na Mboliboli kupitia mikataba mitano.
Alisema mikataba minne imefikia kati ya asilimia 95 na 99 ya utekelezaji na tayari sehemu kubwa ya miundombinu inatumika, huku mkataba wa tano unaohusu ujenzi wa kinga dhidi ya mafuriko ukiwa umefikia asilimia tano.
Akonaay alisema mradi huo unalenga kuongeza eneo la umwagiliaji kutoka hekari 4,500 zilizokuwa zikilimwa awali hadi kufikia hekari 15,000, hatua itakayoongeza uzalishaji wa mazao na kuchochea ukuaji wa uchumi wa wananchi wa Pawaga na Taifa kwa ujumla.
Aliongeza kuwa pamoja na ujenzi wa banio, mifereji mikuu, mifereji ya kati, barabara za mashambani na miundombinu mingine ya umwagiliaji, Tume ya Taifa ya Umwagiliaji imetoa shilingi milioni 212 kwa ajili ya kuwatambua wakulima, kupima mashamba yao na kuwaandalia hati za umiliki.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Iringa, Daud Yassin, alisema chama kimeridhishwa na maendeleo ya mradi huo na hatua zinazochukuliwa na Serikali kuhakikisha wakulima na wafugaji wanaendelea kunufaika bila migogoro.
Alisema Serikali imeweka mpango wa kujenga malambo kwa ajili ya mifugo ili kulinda miundombinu ya umwagiliaji, huku zoezi la upimaji wa mashamba na utoaji wa hati likiwa linalenga kuhakikisha wananchi wa Pawaga wanabaki kuwa wanufaika wakuu wa uwekezaji huo.
Yassin alisema mradi huo, ambao thamani yake sasa imeongezeka hadi kufikia takribani shilingi bilioni 70, ni uwekezaji mkubwa wa Serikali unaotarajiwa kubadilisha uchumi wa Pawaga, Mkoa wa Iringa na Taifa kwa kuongeza uzalishaji wa mpunga na kukuza shughuli za uchakataji wa mazao ndani ya eneo hilo.