Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Mhe. Hamza S. Johari, amesisitiza Mawakili wa Serikali kuendeleza nidhamu, uwajibikaji na uadilifu katika kutekeleza majukumu yao ya kila siku. Hayo ameyasema katika Uchaguzi wa viongozi wa Chama cha Mawakili wa Serikali (TPBA) uliofanyika tarehe 14 Julai 2026 katika Ukumbi wa Mikutano wa Kimataifa Arusha (AICC), Jijini Arusha.

Katika hotuba yake, Mhe. Johari alieleza kuwa chama hicho ni chombo muhimu katika kulinda maslahi ya umma na kuhakikisha sheria zinazingatiwa kwa ufanisi. Aidha, aliwapongeza Mawakili wa Serikali kwa kufanya kazi kwa weledi na kujenga hoja zenye nguvu, akiwataka wasikubali kupotoshwa na waendelee kutekeleza majukumu yao kwa uadilifu na moyo wa kujituma.

Awali, akitoa shukrani kwa wanachama wa TPBA, Bw. Bavoo Junus, Rais mstaafu wa chama hicho, aliwapongeza wanachama kwa mshikamano wao katika kipindi chote cha Uongozi wao, na kuuomba uongozi mpya kuendeleza misingi ya mshikamano na maadili ya kitaaluma ambayo chama kimekuwa kikisimamia kwa muda mrefu.

Kwa upande wake, Rais mpya wa TPBA aliyechaguliwa, Bw. Bonaventure Mwambaja, aliahidi kuendeleza kazi nzuri iliyofanywa na viongozi waliopita. Akisisitiza ajenda ya kuimarisha mafunzo endelevu kwa wanachama na kushirikiana kwa karibu na taasisi za serikali pamoja na wadau wengine wa sekta ya sheria.

Uchaguzi wa viongozi wa Chama cha Mawakili wa Serikali TPBA umefanyika kikamilifu na kupatikana viongozi watakaoongoza chama kwa muda wa Mwaka Mmoja, ambapo Rais aliyechaguliwa ni Bw. Bonaventure Mwambaja, Makamu Rais Acley F. Chaura, Mwenyekiti, Selestina Kunambi, Makamu Mwenyekiti, Farida Kiobya, Katibu, Salmin Shemndolwa na Mweka Hazina ni Frank Ong’eng’a.