Mwanasheria Mkuu wa Serikali Mhe. Hamza S. Johari amefungua mafunzo ya tatu ya Bespoke kwa Mawakili wa Serikali, yalioandaliwa na kuratibiwa na Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali ambayo yameanza tarehe 15 Julai, 2026 na yatahimishwa tarehe 17 Julai, 2026 katika Ukumbi wa Kimataifa wa Mikutano Arusha (AICC) Jijini Arusha.
Mhe. Johari amewasisitiza Mawakili wa Serikali kuhakikisha wanasimamia vyema Utawala wa Sheria katika maeneo yao ikiwa ni pamoja na kuishauri Serikali ipasavyo kuendelea kuzingatia sheria ili kufikia malengo ya Dira ya Taifa 2050.
*“Nitumie fursa hii kuwakumbusha washiriki wote kuwa, tunapoendelea katika kufikia malengo ya Dira ya Taifa 2050 ni muhimu kufahamu kuwa, Taifa linahitaji zaidi ya utaalamu wetu wa sheria.”* Amesema Mwanasheria Mkuu wa Serikali.
Aidha, Mhe. Johari amewakumbusha Mawakili wa Serikali kutambua nafasi yao katika utekelezaji wa Dira ya Taifa 2050, ambapo ameeleza kuwa utekelezaji wa malengo ya yake unategema kwa kiwango kikubwa uwezo wa Mawakili wa Serikali, pamoja na kuwa na mifumo ya kisheria itakayokwenda sambamba na kasi ya maendeleo na mabadiliko yanayoendelea nchini na duniani kote.
*“Ni imani yetu kuwa, Dira hii itatekelezwa kwa kiwango kilichokusudiwa kwa kupitia Sheria bora, Sera madhubuti, Mikataba yenye tija, Mifumo bora ya utawala wa kisheria sambamba na taasisi zenye uwezo wa kutafsiri malengo ya maendeleo kuwa matokeo yanayoonekana kwa manufaa ya Taifa lote kwa ujumla.”* Amesema Mwanasheria Mkuu wa Serikali.
Katika hatua nyingine, Mwanasheria Mkuu wa Serikali amewahimiza Mawakili wa Serikali kuzingatia matumizi ya teknolojia ambayo yamebadilisha kwa kiasi kikubwa utoaji wa huduma za kisheria ikiwemo matumizi ya *Akili Mnemba* na utoaji wa matumizi ya Ushahidi wa Kielektroniki.
*“Mapinduzi ya teknolojia yamebadilisha kwa kiasi kikubwa, namna ambavyo huduma za kisheria zinaendelea kutolewa nchini na duniani kote kwa ujumla, hivyo katika mazingira haya, Mawakili wa Serikali na Maafisa Sheria hawawezi kuendelea kutekeleza majukumu yao ya kazi kwa kutumia mazoea ya zamani”.* Amesema Mhe. Johari.
Vilevile, Mhe. Johari amewataka Mawakili wa Serikali kuendelea kufanya kazi kwa kuzingatia Uadilifu, Weledi, Uwajibikaji, Uzalendo na Nidhamu ili waweze kutoa ushauri wenye ubora na tija na Mikataba yenye manufaa kwa Taifa.
*“Wananchi wanatarajia kuona rasilimali za umma zikilindwa kwa wivu mkubwa. Wananchi wanatarajia kuona Sheria zikitumika kama nyenzo ya maendeleo ya kufikia malengo ya Dira ya Taifa 2050.”* Amesema Mhe. Johari.
Mwanasheria Mkuu wa Serikali ametoa wito kwa Mawakili wa Serikali kuendelea kuyatumia mafunzo haya kama fursa ya kujifunza, kubadillishana uzoefu, kujenga mitandao ya kitaaluma, kuibua suluhisho za changamoto zinazowakabili Mawakili hao.
Kwa upande wake, Gavana Mstaafu wa Benki Kuu ya Tanzania (BOT), Prof. Florens Luoga akitoa mada kuhusu *”Nafasi ya Kimkakati ya Mawakili wa Serikali katika kufikia Dira ya Taifa 2050,*” ambapo ameeleza nafasi waliyonayo Mawakili wa Serikali katika kufanya maboresho mbalimbali ya Kisheria ili kuweza kutimiza malengo ya Dira 2050.
*“Wakili wa Serikali ana nafasi kubwa katika kuchangia maendeleo ya nchi na kulinda maslahi ya Taifa, kwakuwa ushauri wa kisheria anaoutoa ni kichocheo katika mageuzi ya kiuchumi.”* Amesema Prof. Luoga
Awali, akimkaribisha Mgeni Rasmi, Mwandishi Mkuu wa Sheria Bw. Onorius Njole alimshukuru Mwanasheria Mkuu wa Serikali kwa kuwezesha kufanyika kwa mafunzo hayo muhimu kwa Mawakili wa Serikali ambayo yataleta mabadiliko katika utekelezaji wa majukumu yao.
Akiwakaribisha washiriki katika mafunzo ya tatu Bespoke, Mkurugenzi wa Uratibu na Huduma za Sheria, Bi. Neema Ringo eamelezea mafunzo haya yatasaidia kuwezesha Mawakili wa Serikali kupata uzoefu katika nyanja mbalimbali za kisheria, ambapo ameeleza kuwa wakufunzi mahiri watawasilisha mada mbalimbali kwa Washiriki wa Mafunzo ya Bespoke.
Msimu wa tatu wa Mafunzo ya Bespoke kwa Mawakili wa Serikali yamefunguliwa tarehe 15 Julai na yataendelea hadi tarehe 17 Julai, 2026 Jijini Arusha ambapo Mawakili wa Serikali wanatarajia kujifunza masuala mbalimbali ya kisheria na kiuchumi kutoka kwa Wakufunzi wabobevu wa Kitaifa na Kimataifa.

